21
Oct

PAC YARIDHIA TFS, YATOA MAAGIZO KUIMARISHA UHIFADHI NA UWAJIBIKAJI

DODOMA: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeelekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu, ufuatiliaji wa mikataba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo kwa manufaa ya Taifa.

Maelekezo hayo yametolewa leo, Oktoba 21, 2026, jijini Dodoma, katika kikao cha Kamati hiyo kilichoongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa PAC, Mhe. Beng’i Mazana Issa, ambaye ameitaka TFS kuhakikisha maagizo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa wakati na kuwasilisha taarifa za maendeleo kwa mamlaka husika.

Katika maagizo yake, Kamati imeitaka TFS kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka na wadau husika kuharakisha taratibu za kisheria na kiutawala zinazohusu hifadhi za misitu na milima, kuimarisha miongozo ya mikataba na kukamilisha masuala ya hati za miliki zilizobaki.

Aidha, TFS imeelekezwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa mikataba ili kuhakikisha kampuni na wadau wanaotekeleza shughuli katika maeneo husika wanatimiza wajibu wao, ikiwemo masharti ya kimazingira, malipo na masharti mengine ya mikataba.

Kamati pia imesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya TFS, Wizara na wadau wa maendeleo katika kufuatilia upatikanaji wa fedha za miradi, kuhakikisha masharti ya utekelezaji yanazingatiwa na fedha zinazopatikana zinatumika kwa wakati ili kukamilisha miradi iliyopangwa.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Ushauri ya TFS, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Luteni Mstaafu Chiku Abdallah Gallawa, amesema Bodi itaendelea kutoa ushauri na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha Wakala unaimarisha utendaji na kupata matokeo chanya.

Gallawa amesema Bodi iko tayari kushirikiana na Kamati na kupokea ushauri unaolenga kuboresha utendaji wa TFS, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano ya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi mwisho wa mwaka wa fedha kabla ya kujadili changamoto zinazojitokeza.