03
Oct

KAMATI YA MISITU DUNIANI YASISITIZA UWEKEZAJI, TEKNOLOJIA UHIFADHI MISITU

Na Mwandishi Wetu – Roma, Italia

Kamati ya Misitu Duniani (COFO) imesisitiza kuimarishwa kwa uwekezaji wa kitaalamu na kifedha katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu, ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa kukabiliana na changamoto za moto, uharibifu wa misitu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha 28 cha COFO kilichofanyika kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 3, 2026, katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Roma, Italia, kilichohudhuriwa na wawakilishi wa nchi wanachama 186, wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na maafisa waandamizi wa sekta ya misitu.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni hali ya rasilimali za misitu duniani, juhudi za kupunguza uharibifu na kurejesha misitu iliyopotea, pamoja na kuimarisha ulinzi wa misitu ambayo bado haijaharibiwa ili kuhakikisha uendelevu wake.

Kikao hicho pia kilijadili mchango wa misitu katika usalama wa chakula na lishe, uwekaji kijani wa miji kupitia upandaji na utunzaji wa miti, kuongeza thamani ya bidhaa za misitu za mbao na zisizo za mbao, pamoja na namna bora ya kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Aidha, wajumbe walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau wengine katika uhifadhi, huku Malipo kwa Huduma za Mazingira (PES) yakitajwa kuwa miongoni mwa mifumo inayoweza kusaidia kuongeza ushiriki na uwekezaji katika uhifadhi.

Baada ya majadiliano, wajumbe walikubaliana juu ya umuhimu wa kuongeza uwezeshaji wa kitaalamu na kifedha kupitia mifuko mbalimbali ya mazingira, huku FAO na wadau wengine wakihimizwa kuunga mkono utekelezaji wa mikakati hiyo.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Seleboni Mushi, Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Misitu, akifuatana na Dkt. Zainabu Bungwa, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali wa TFS, na Dkt. Emmanuel Masenga, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti (TAWIRI).

Katika maadhimisho ya Wiki ya 10 ya Misitu Duniani yaliyofanyika sambamba na kikao hicho, ujumbe wa Tanzania uliwasilisha mazao ya nyuki na kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa misitu, mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki na bidhaa nyingine zisizo za mbao zinazotokana na rasilimali za misitu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Bungwa alisema Serikali, taasisi za uhifadhi na wadau wanaweka mkazo katika kuendeleza sekta ya nyuki kutokana na mchango wake katika kuongeza kipato cha jamii, kuboresha lishe na kusaidia uhifadhi wa misitu, ikiwemo kupunguza uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo.

Kwa upande wake, Mushi aliwahakikishia wajumbe wa COFO kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na FAO na wadau wengine katika kufuatilia fursa zilizowasilishwa na kutekeleza mikakati iliyokubaliwa, ikiwemo kubadilishana utaalamu, tafiti, teknolojia za kisasa na kuimarisha uwezeshaji wa miradi ya uhifadhi wa misitu.