15
May

TEKNOLOJIA YA SATELAITI YAISAIDIA TFS KUPUNGUZA MOTO WA MISITU KWA ASILIMIA 11

-Mafunzo kwa wananchi na vikosi vya moto yaongeza usalama wa hifadhi-

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

JUHUDI za Serikali za kutumia teknolojia ya satelaiti kufuatilia moto wa misitu zimeanza kuzaa matunda baada ya matukio ya moto kupungua kwa wastani wa asilimia 11 kwa mwaka.

Katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2026/2027 iliyosomwa bungeni Dodoma Mei 15, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii (Mb), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema TFS imeendelea kuimarisha mifumo ya kudhibiti moto kwa kusafisha kilomita 2,723 za njia za kuzuia moto na kusimamia minara 17 ya kuangalia matukio ya moto.

Aidha, vituo saba vya kufuatilia na kudhibiti moto vinaendelea kufanya kazi katika maeneo ya hifadhi.

Katika kipindi hicho, vikosi 45 vyenye askari na wadau 705 vilipatiwa mafunzo ya kukabiliana na moto huku wananchi 20,297 kutoka vijiji 245 vinavyopakana na hifadhi wakipatiwa elimu ya udhibiti wa moto.

Mhe. Dkt. Kijaji alisema matumizi ya teknolojia ya satelaiti yameiwezesha TFS kubaini matukio ya moto mapema kabla hayajasababisha madhara makubwa.
Katika mpango wa mwaka 2026/2027, TFS imepanga kufanya kampeni 295 za kuzuia moto katika vijiji 337 na kuunda vikundi 49 vya udhibiti wa moto.

Pia, minara mitatu mipya itajengwa katika Mashamba ya Miti ya Silayo, Buhigwe na Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia wa Pugu/Kazimzumbwi.

Kwa Takwimu
* Njia za kuzuia moto zilizosafishwa: Km 2,723
* Minara ya moto inayotumika: 17
* Wananchi waliopatiwa mafunzo: 20,297
* Vijiji vilivyofikiwa: 245
* Upungufu wa matukio ya moto: 11%