26
Nov
Dkt. Tulia Aongoza Kampeni ya Upandaji Miti Milioni Mbili Kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, ametoa wito kwa jamii kuzingatia matumizi ya nishati safi na kuchukua hatua za kutunza mazingira kupitia upandaji wa miti rafiki.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti leo, Novemba 25, 2024, Dkt. Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), alieleza kuwa lengo ni kupanda miti milioni mbili ya kivuli inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kampeni hii, inayohusisha Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), inalenga kuhamasisha wananchi wa Mkoa wa Mbeya, na imehusisha upandaji miti katika shule za msingi na sekondari, huku ikigusa kata 36.
Dkt. Tulia alisisitiza kuwa, "Hii ni awamu ya pili ya kampeni yetu. Awamu ya kwanza tulipanda miche ya matunda 8,000, na sasa tumejizatiti kupanda miti ya vivuli milioni mbili. Tutaendelea kushirikiana na TFS katika juhudi hizi."
Aidha, Dkt. Tulia aliiomba TFS kutoa miti kwa ajili ya kupanda katika eneo la Mlima Kawetele, ambalo lina changamoto ya mazao kutostawi.
Alisisitiza umuhimu wa kufanya utafiti ili kuona ni aina gani ya miti inaweza kustawi katika eneo hilo, ambayo itaweza kuhudumiwa na kuvunwa kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano.
Kwa upande wake, Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, alieleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda rasilimali za misitu.
Alisisitiza kuwa misitu ni muhimu kwa mazingira yetu kwani hutoa kivuli, matunda, mbao, na kusaidia kulinda viumbe hai na rasilimali ya maji.
"Spika Dkt. Tulia anafanya kazi kubwa ya kuhamasisha utunzaji wa misitu ya asili na tunamshukuru kwa juhudi zake katika kuhimiza sheria za uhifadhi wa mazingira," alisema Prof. Silayo.
Chifu wa Mkoa wa Mbeya, Rocket Mwansinga, aliongezea kuwa machifu wanayo jukumu muhimu katika kulinda rasilimali za misitu na kuepuka uharibifu wa mazingira.
Aliwataka wananchi na viongozi wa kijamii kushirikiana na TFS katika kulinda misitu ya asili ili kuepuka athari za kupotea kwa rasilimali za maji.
"Tumepewa amri na serikali kutunza misitu ya asili, na tutaendelea kushirikiana na TFS kuhakikisha tunazuia waharibifu wanaokata miti ovyo," alisema Chifu Mwansinga.
Kampeni ya upandaji miti milioni mbili ni hatua muhimu katika jitihada za Tanzania kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, huku ikilenga kuhakikisha usalama wa mazingira na uendelevu wa rasilimali za misitu kwa vizazi vijavyo.