01
Jul

TFS Kuuza Miti ya Misaji Kwa Mnada wa Kielektroniki Julai

Dodoma. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetangaza kufanya mauzo ya miti aina ya misaji yenye jumla ya meta za ujazo 6,480.31 kwa njia ya mnada wa kielektroniki, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ufanisi katika biashara ya mazao ya misitu hapa nchini.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, mauzo hayo yatafanyika katika mashamba mawili ya miti yaliyoko Longuza, Muheza mkoani Tanga na Mtibwa, Turiani mkoani Morogoro.

Shamba la miti Longuza linatarajiwa kuuza meta za ujazo 1,757.36 huku Shamba la miti Mtibwa likitarajia kuuza meta za ujazo 4,722.95, na kufanya jumla ya ujazo wote kufikia meta za ujazo 6,480.31.

Mnada huu utafanyika kwa njia ya mtandao kwa kuzingatia Kanuni ya 31(ii) ya Kanuni za Misitu za mwaka 2004. TFS imeweka ratiba ya mnada kuwa Alhamisi tarehe 17 Julai, 2025 kwa Shamba la Longuza kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tano na dakika nne asubuhi, na Ijumaa tarehe 18 Julai, 2025 kwa Shamba la Mtibwa kwa muda sawa.

Usajili na Ukaguzi

Wadau wanaotaka kushiriki mnada huu wanatakiwa kujisajili kupitia mfumo wa mnada wa kielektroniki wa TFS kupitia anuani http://mis.tfs.go.tz/e-auction kuanzia tarehe ya tangazo hadi Jumanne tarehe 15 Julai, 2025 saa tisa kamili mchana. Kwa msaada wa usajili, TFS imetoa namba za mawasiliano: +255 766 924 232 na +255 766 857 062.

Aidha, washiriki wanahimizwa kwenda kukagua miti inayouzwa katika mashamba husika kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa alasiri siku za Jumatatu hadi Ijumaa, isipokuwa siku za sikukuu, hadi tarehe 15 Julai, 2025.

Masharti na Taratibu

Prof. Silayo amesema mnunuzi anapaswa kuhakikisha anafuata masharti yote yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kuthibitisha ushiriki wake angalau dakika tano kabla ya mnada kuanza. Malipo yote yatafanyika kwa njia ya benki au mitandao ya watoa huduma za kifedha kupitia Mfumo wa Makusanyo ya Serikali (GePG).

Mnunuzi atakayeshinda atanunua kwa masharti ya kulipa asilimia 25 ya thamani ya ununuzi ndani ya siku tatu na kumalizia malipo yaliyosalia ndani ya siku 14. Pia, mnunuzi hataruhusiwa kusafirisha magogo nje ya nchi na anatakiwa kuondoa mazao ndani ya siku 60 baada ya kumaliza malipo yote.

Ploti za miti zimegawanywa katika mafungu na kila fungu litauzwa ndani ya saa moja huku kukiwa na mapumziko mafupi ya dakika mbili kati ya fungu moja na lingine.

Fursa na Uwajibikaji

Prof. Silayo amesema hatua hii inalenga kuimarisha uwazi, kuongeza mapato ya serikali na kuchochea biashara endelevu ya mazao ya misitu nchini. Ameongeza kuwa TFS itatoa barua za ushindi na hati za madai kwa wanunuzi waliofanikiwa mara baada ya mnada kukamilika.

Tangazo hili limechapishwa pia katika tovuti ya TFS www.tfs.go.tz na linapatikana kwa umma kwa ajili ya taarifa na maandalizi ya ushiriki.


Mwisho

Download File/s: