20
Oct

DC SHINYANGA ATOA WITO WA KUONGEZA JUHUDI KATIKA UFUGAJI NYUKI

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka maafisa na askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuongeza bidii na ubunifu katika usimamizi wa rasilimali za nyuki ili kuongeza uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki nchini.

Mtatiro ametoa wito huo Oktoba 20, 2026, wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa manzuki na makundi ya nyuki kwa maafisa na askari wa TFS kutoka kanda saba nchini, yanayolenga kuongeza ujuzi na maarifa ya usimamizi wa nyuki na uzalishaji wa mazao yake.

Amesema watumishi hao wana nafasi muhimu katika kuendeleza sekta ya nyuki na wanapaswa kutumia maarifa na ubunifu kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

“Nyinyi ni askari ambao bado ni vijana wadogo, kwa hiyo mna muda mrefu wa kuisaidia taasisi na taifa katika sekta ya ufugaji nyuki kwa kuongeza nguvu na ubunifu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya nyuki nchini,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa Rasilimali za Nyuki wa TFS, Hussein Msuya, amesema mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo wa watumishi na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa manzuki na kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki.

Msuya amesema TFS inalenga kuongeza uzalishaji wa asali kwa asilimia 15 kila mwaka kutoka tani 45 zinazozalishwa kwa mwaka kwa sasa hadi kufikia angalau tani 90 kwa mwaka ndani ya miaka mitano ijayo.

Baadhi ya washiriki wamesema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi wa kuboresha uzalishaji wa nyuki na kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na nyuki.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu na yanawakutanisha maafisa na askari wa TFS kutoka kanda saba nchini.