02
Dec
Afrika yaonywa kuchukua hatua haraka kulinda misitu, wanyamapori
Banjul, Gambia, 1 Desemba 2025 — Viongozi wakuu wa sekta ya misitu na wanyamapori barani Afrika wamefungua Mkutano wa 25 wa Tume ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC25) pamoja na Wiki ya 9 ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW9) hapa Banjul, wakiwahimiza nchi zote kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa misitu na vitisho kwa wanyamapori.
Hayo yamesemwa wakati wa ufunguzi wa kikao cha 25 cha African Forestry and Wildlife Commission (AFWC25) na Wiki ya tisa ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW9) kilichofanyika Banjul, jana.
Mkutano huo wa wiki moja, unaoandaliwa na Serikali ya Gambia kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), umevuta mawaziri, wataalamu, taasisi za kimataifa na wadau wa uhifadhi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Mwakilishi wa FAO Kanda ya Afrika, Dk Abebe Haile-Gabriel, aliipongeza Gambia katika kurejesha misitu na usimamizi endelevu wa ardhi.
Aliahidi kuendelea kusaidia nchi wanachama kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa misitu, uhifadhi wa mikoko, mpango wa Great Green Wall na miradi ya jamii ya bayoanuai.
Hata hivyo, alionya kuwa bara linaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa linalochochewa na tabianchi.
“Afrika inahitaji fedha bunifu, sera madhubuti na ushirikiano wa kikanda ili kulinda rasilimali zake za asili,” alisema.
“Kikao hiki kinatubebesha wajibu wa kujenga mustakabali wenye ustahimilivu zaidi.”
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Gambia, Mandisa Mashologu, alisema athari za tabianchi tayari zimeanza kuathiri upatikanaji wa maji, chakula na kipato katika mataifa mengi ya Afrika.
Alisema UNDP inaendelea kusaidia nchi katika kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, maandalizi ya majanga, nishati mbadala na urejeshwaji wa mifumo ikolojia.
Akiwakilisha Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa AFWC, Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS, Prof. Dos Santos Silayo wa Tanzania, Naibu Mwenyekiti Bw. Dieudonne Sita aliipongeza Gambia kwa kuandaa kikao hicho baada ya Mali kushindwa kufanya hivyo.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘simamizi shirikishi na bunifu wa misitu na wanyamapori barani Afrika’ inahitaji nchi kushirikiana kwa karibu na kubadilishana ujuzi.
Alibainisha kuwa maazimio ya kikao cha Banjul yatatumika kuiweka Afrika katika nafasi moja ya kimkakati kuelekea majadiliano ya kimataifa kuhusu misitu na maandalizi ya Mkutano wa FAO wa Kanda ya Afrika unaotarajiwa Aprili 2026.
Shughuli za siku ya kwanza zilihusisha hotuba za ufunguzi na wito wa kuongeza hatua za kulinda misitu, wanyamapori na jamii zinazokabiliwa na athari za tabianchi.