27
Oct

WANANCHI URAMBO WAMILIKISHWA ARDHI KWA HATI 333 KUPITIA MRADI WA DSL-IP

Na Mwandishi Wetu, Tabora 

Serikali imekabidhi hati za hakimiliki za kimila 333 kwa wananchi wa Kijiji cha Tumaini, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo (DSL-IP) unaoratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ukiwa na lengo la kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kupunguza migogoro kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hati hizo jana Octoba 25,2025, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dk. Hamisi Mkanachi, alisema hatua hiyo itawawezesha wananchi kuwekeza katika shughuli endelevu za kilimo, ufugaji na biashara za mazao ya misitu, hatua itakayoongeza kipato cha kaya na kulinda mazingira. “Katika nchi yetu ambako uchumi unategemea sana rasilimali asilia kama ardhi, misitu na maji, hati hizi zitasaidia kupunguza migogoro kati ya wananchi na hifadhi, kwa sababu kila mmiliki atajua mipaka yake inaishia wapi,” alisema Dk. Mkanachi. 

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TFS, Hussein Msuya (SACC), alisema mradi huo wenye thamani ya dola milioni 6.8 za Marekani (takriban Sh bilioni 16.8) unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2023–2027) katika wilaya za Kaliua, Urambo, Sikonge (Tabora) na Mlele (Katavi). Alisema lengo ni kurejesha uoto wa asili, kupunguza uharibifu wa ardhi na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na misitu ya miombo. “Mradi huu ni sehemu ya jitihada za kimataifa zinazotekelezwa katika nchi 11 ikiwemo Tanzania, Kenya, Malawi, Zimbabwe na Angola. Umeanza kwa kutambua vikundi vya wazalishaji wa mazao ya misitu na mashamba (FFPOs) ili waweze kunufaika kiuchumi kupitia uhifadhi endelevu,” alisema Msuya. Msuya aliongeza kuwa tangu mwaka 2018, TFS imewezesha mipango ya matumizi bora ya ardhi 114, na kati ya hiyo, mipango 14 imekamilika kupitia mradi wa DSL-IP.

 Alisema lengo ni kuongeza idadi ya hati hadi zaidi ya mara tano kabla ya mradi kuhitimishwa mwaka 2027. Aidha, TFS imeanza manunuzi ya vitendea kazi vya kisasa kama ndege nyuki (drone) pamoja na kutoa mafunzo kwa vikundi vya jamii na watumishi wa wilaya ili kuboresha upangaji wa matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa misitu. Baadhi ya wananchi waliopatiwa hati walishukuru Serikali kwa kuwapatia milki halali ya ardhi, wakisema hatua hiyo imeongeza ulinzi wa mali zao na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Jumla ya hati 333 zilitolewa, zikiwemo za wanaume 212, wanawake 97 na hati za pamoja 24.