
04
Mar
Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS, Dkt. Abel Masota, Asisitiza Umuhimu wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo
Tabora, Machi 3, 2025 – Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Abel Masota, akimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, amesisitiza umuhimu wa usimamizi shirikishi wa misitu ya Miombo ya Nyanda Kame katika kuhakikisha uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu na ardhi nchini.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Wataalam wa Mradi wa Integrated Landscape Management in the Dry Miombo Woodlands of Tanzania, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JM Hotel, Tabora, Dkt. Masota alibainisha mafanikio na matarajio ya mradi huo.
Mradi huu, unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Unalenga kukabiliana na changamoto za uharibifu wa ardhi na kupotea kwa bioanuwai katika maeneo ya Tabora (Kaliua, Sikonge, Urambo) na Katavi (Mlele). Ukiwa na thamani ya dola milioni 6.87, mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2022-2027) na unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa misitu.
"Lengo letu ni kuhakikisha misitu ya Miombo inalindwa kwa ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo jamii za maeneo husika. Kupitia mradi huu, tunatarajia kupunguza uharibifu wa ardhi na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo," alisema Dkt. Masota.
Aidha, alitaja mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa mradi huo kuwa ni pamoja na mafunzo ya kitaifa kuhusu mbinu bora za kupunguza uharibifu wa ardhi, ununuzi wa vitendea kazi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi, na kuanzishwa kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 14 vya Tabora na Katavi. Vilevile, mradi umechangia uboreshaji wa uwezo wa wataalam kutoka sekta za misitu, kilimo, mifugo, na maji, pamoja na utoaji wa hati miliki za kimila kwa vijiji vinavyohusika na uhifadhi wa misitu, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.
Katika hate nyingine, Dkt. Masota alihimiza kuongezwa kwa juhudi za kuhifadhi misitu kwa kuzingatia fursa kama ufugaji wa nyuki, nishati safi, na utalii ikolojia, ambazo zinaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa jamii kwa misitu kwa njia endelevu.
“Ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na jamii ni muhimu kwa mafanikio ya mradi huu. Tunapaswa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uhifadhi wa misitu na maendeleo endelevu, alihitimisha Dkt. Masota.
Mwakilishi wa FAO na Mratibu wa Mradi, Bw. Jonathan Sawaya, alishukuru kwa mwitikio mkubwa ulioonyeshwa kutoka kwa viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais - TAMISEMI, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), pamoja na wadau kutoka sekta za kilimo, mifugo, na maji.
Alisema kuwa mradi huu ni wa shirikishi, na kwamba Tanzania imepewa jukumu la kuwa kinara wa shughuli za ufugaji nyuki, hivyo nchi zote zilizosalia zinategemea kuja kujifunza kutoka kwa Tanzania katika eneo hilo.
Aidha, alibainisha kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni eneo lingine ambalo Tanzania inaongoza, na akawahimiza wadau kutumia kikao hicho kujadili masuala ya kitaalamu ili kufanikisha malengo ya mradi huo.