09
Sep

Mradi wa Miombo, kuzingatia usawa wa kijinsia na fursa shirikishi

Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo nchini Tanzania, unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa thamani ya shilingi bilioni 16.8, utazingatia masuala ya kijinsia na ushirikishaji wa jamii katika kila hatua ya utekelezaji.

Akitoa wasilisho kwenye mafunzo kuhusu masuala ya jinsia yaliyofanyika tarehe 4-6 Septemba, 2024, Jijini Nairobi, Afisa Kiungo Mwandamizi wa Mradi, Linda Shio, alisema kuwa Tanzania imezingatia umuhimu wa masuala ya jinsia na ushirikishaji wa makundi yote tangu mwanzo wa mradi.

Bi. Shio alisema, "Mpaka mradi utakapokamilika Desemba 2027, tunatarajia Mpango Kazi wa Masuala ya Kijinsia utajibu matarajio yaliyowekwa, ikiwemo kuwezesha wanawake kushiriki katika shughuli za ufugaji nyuki, mnyororo wa thamani wa mzao ya nyuki, na kilimo."

"Aidha, mradi unalenga kuwezesha wanawake katika nyanja zote, kuanzia mipango ya matumizi bora ya ardhi na usimamizi endelevu wa ardhi na misitu, hadi matumizi ya mbegu bora za kilimo na miti," anasema.

Awali, Mratibu wa Mradi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – TFS, Zainabu Shabani Bungwa, alisema kuwa Mradi wa Miombo unatekelezwa kwa muda wa miaka mitano na unalenga kukomesha uharibifu wa ardhi na upotevu wa bionuwai katika maeneo yaliyoharibiwa ya ukanda wa Misitu ya Miombo Kusini Magharibi mwa Tanzania kwa njia shirikishi.

"Kati ya nchi 11 zinazoshiriki, kila nchi itapimwa kwa lengo lake lililojiwekea. Kwa Tanzania, kipimo kitakuwa uzalishaji endelevu wa asali ya Miombo," anasema.

Aidha, mradi utaendeshwa katika ukanda wa Tabora (Kaliua, Sikonge, na Urambo) na Katavi (Mlele). Wizara ya Maliasili kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) inashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira kupitia Mfuko wa Mazingira (GEF), pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Washiriki wengine kutoka Tanzania waliohudhuria kikao hicho ni Johary Kachwamba anayesimamia Uelimishaji na Mawasiliano na Deogratias Malogo anayesimamia Ufuatiliaji na Tathimini.