23
Aug

TFS YAPONGEZWA KWA KAZI NZURI YA ULINZI WA MISITU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa jitihada zake za kulinda maeneo ya misitu nchini na kuwasisitiza kuwa wabunifu na kuongeza mashamba ya miti.

Mhe. Chana ameyasema hayo leo Agosti 23,2024 wakati wa kikao na Menejimenti, Maafisa na Maaskari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)kilichofanyika Makao makuu ya TFS Misitu House Itega jijini Dodoma.

“Hongereni kwa kazi nzuri za ulinzi mzuri wa misitu na uhifadhi, kuna mvua za kutosha, chakula cha kutosha na ninawaahidi ushirikiano wa kutosha na milango yangu iko wazi” amesema Mhe. Chana.

Aidha, ameitaka TFS kuwa mfano bora wa kuigwa katika masuala ya uhifadhi na utunzaji wa misitu na kutumia teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao akitolea mfano matumizi ya ndege nyuki “drones”na helikopta.

Pichani: Kamishna wa Uhifadhi TFS akielezea jambo wakati wa ziara ya Waziri Mhe. Pindi Chana katika ofisi za makao Makuu ya TFS Itega-Dodoma;

“Tusikubali misitu ipungue kwa sababu tumepewa dhamana ya kuisimamia, ulinzi wa maeneo tuliyokabidhiwa ni wajibu wetu” amesema Mhe. Chana.

Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya uhifadhi na kuwa mhifadhi namba moja na kuitaka  TFS kubuni na kuongeza mazao mapya ya utalii, ili kuendeleza juhudi za Mheshimiwa Rais.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amewasilisha taarifa ya utendaji ya TFS kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 na mwelekeo wa TFS kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 na kukiri kupokea maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi.