23
Sep
TFS YAPONDEZWA UHIFADHI BUKOMBE, WILAYA YATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KABONI
FS YAPONDEZWA UHIFADHI BUKOMBE, WILAYA YATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KABONI
BUKOMBE. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa juhudi za uhifadhi wilayani Bukombe, huku akitaka eneo hilo kutumia fursa ya biashara ya kaboni kutokana na ukubwa wa maeneo ya hifadhi.
Mhe. Kwagilwa ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Septemba 22, 2026, wakati wa ziara yake wilayani Bukombe, mkoani Geita, akisema asilimia 78 ya eneo la wilaya hiyo ni maeneo ya hifadhi yanayoweza kutoa fursa kwa wananchi na Serikali kunufaika na biashara ya kaboni.
Ameitaka Serikali ya Wilaya kuwasiliana na kituo kinachoratibu biashara ya kaboni ili kutathmini namna wananchi na Serikali wanavyoweza kunufaika na shughuli hiyo inayohusisha uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za misitu.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri amepongeza juhudi za TFS katika kupanda miti na kulinda maeneo yaliyohifadhiwa, akisisitiza kuwa uhifadhi huo unapaswa kwenda sambamba na ufuatiliaji wa miche inayopandwa.
Amesema upandaji wa miti pekee hautoshi iwapo miche hiyo haitasimamiwa hadi ikue, akitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha miche inayopandwa inatunzwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza uoto wa miti na kulinda mazingira.
“Miti mingi inapandwa lakini haikui kutokana na kutosimamiwa vyema, hivyo ni muhimu kuhakikisha miche inayopandwa inafuatiliwa mpaka ikue,” amesema.
Mhe. Kwagilwa pia ameipongeza Wilaya ya Bukombe kwa hatua za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwamo ugawaji wa mitungi ya gesi kwa wananchi, akisema matumizi hayo yanaweza kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa na hivyo kupunguza shinikizo kwenye misitu.
Amesema juhudi za uhifadhi zinapaswa kuhusisha pia hatua za kupunguza matumizi ya nishati zinazochangia uharibifu wa misitu, huku matumizi ya nishati safi yakihamasishwa zaidi kwa wananchi.