26
Oct

Tanzania Yajiandaa kwa Mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki 2027

---𝗬𝗮𝗮𝗻𝘇𝗮 𝘂𝗵𝗮𝗺𝗮𝘀𝗶𝘀𝗵𝗮𝗷𝗶 𝗸𝘂𝗽𝗶𝘁𝗶𝗮 𝗡𝘆𝘂𝗸𝗶 𝗠𝗮𝗿𝗮𝘁𝗵𝗼𝗻 𝗔𝗿𝘂𝘀𝗵𝗮

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amewataka wananchi na wadau wa ufugaji nyuki nchini kuchangamkia fursa ya Mkutano wa Dunia wa Ufugaji wa Nyuki (Apimondia) utakaofanyika mwaka 2027.

Akizungumza katika Nyuki Marathon iliyofanyika leo Oktoba 26,2024 Jijini Arusha, Prof. Silayo alisisitiza kwamba ufugaji nyuki si tu ni biashara bali pia unachangia katika ukuzaji wa utalii na uhif-dhi.

Marathoni hiyo ilihusisha wanariadha takriban 500 kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa na lengo la kuhamasisha ufugaji wa nyuki na kutangaza umuhimu wa mazingira.

Prof. Dos Santos alisisitiza kuwa mashindano hayo ya Nyuki marathon ni ya kwanza duniani na mashindano muhimu kwa afya, ukuwaji wa sekta ya nyuki nchini na duniani sambamba na kujenga mahusiano mema ya nchi yetu kimataifa kwa sababu yameleta watu wa mataifa mbalimbali kuja kushiliki mashindano hayo.

"Lakini kwakuwa tunajiandaa kama sehemu ya kufanyika kwa Kongress ya 50 ya Apimindia 2027 hapa nchini imekuwa sehenu nzuri sana yakutuma ujumbe kwamba Tanzania tuko tayari, " anasema.

Anaongeza kuwa utunzaji mzuri wa mazingira unachangia katika uzalishaji wa nyuki, na hivyo kuongeza uchumi wa jamii. "Nyuki ni mtaji; wanapaswa kutunzwa kwa kutumia mizinga na mazingira lazima yalindwe," alisema.

David Mukomana, Rais wa Kamati ya Kanda ya Apimondia kwa Afrika, alisisitiza umuhimu wa tukio hili kama jukwaa la kuhamasisha ufahamu kuhusu ufugaji nyuki. Alieleza, "Nyuki Marathon ni hatua muhimu kuelekea mwaka 2027. Tunaweza kujenga ustahimilivu wa jamii kupitia ufugaji nyuki."

Mukomana alieleza uhusiano wake wa kibinafsi na tukio hili, akisema, "Nyuki Marathon ni jambo la pekee sana kwangu. Linawakilisha hatua muhimu kuelekea mwaka 2027, natambua uwepo wa Meya wa Arusha kama ishara ya kuonyesha utayali wa jiji hili  na Tanzania kuelekea kongamano lijalo."

Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, alitangaza mpango wa kugawa mizinga milioni 2, akisisitiza lengo la kuongeza idadi ya nyuki katika eneo hilo. "Tunataka Arusha iwe na nyuki wengi; mkutano wa Apimondia utakuwa chachu katika kuleta maendeleo," alisema.

Wakati huo huo, Restetuta Lopes Lazarus, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Woker Bees Africa, aliongeza kwamba mbio hizo zililenga kuelezea umuhimu wa nyuki kwa maisha ya binadamu, akisisitiza kwamba asali ni tiba kwa magonjwa mbalimbali.

Marathoni hiyo, iliyopewa kauli mbiu "Kuelekea Apimondia 2027," ilidhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa ndani na wa kimataifa katika kukuza ufugaji wa nyuki na kulinda mazingira.