26
Sep
GOP YAHAIDI KUSHIRIKIANA NA TFS KUTANGAZA UTALII IKOOLOJIA
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwanzilishi mwenza wa Mradi wa Guardians of Peak (GOP) chini ya Kampuni ya RAM Film Production, Elizabeth Mrembo, ameahidi kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kutangaza vivutio vya utalii ikolojia vilivyopo nchini ndani na nje ya Tanzania.
Mrembo alitoa ahadi hiyo Septemba 26, 2026, alipotembelea banda la TFS katika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam, ambako yanafanyika maonesho ya Wiki ya Utalii kuelekea kilele cha Siku ya Utalii Duniani 2026.
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii na itaendelea kutumia fursa mbalimbali kutangaza vivutio vya utalii ikolojia vya Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Kampuni yetu inashirikiana na Wizara ya Maliasili kwa ukaribu sana na ninaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutangaza vivutio vya utalii ikolojia nje ya Tanzania,” alisema Mrembo.
Mbali na kutangaza vivutio vya utalii, Mrembo alisema GOP itaendelea kushirikiana na TFS katika kuhamasisha jamii kuhusu upandaji miti na utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii.
Alisema mradi huo pia una kampeni ya upandaji miti, ambapo Oktoba 7, 2026, wanatarajia kwenda Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya zoezi hilo kwa kushirikiana na wahifadhi wa eneo hilo.
“Pamoja na kutangaza utalii, sisi pia tuna kampeni ya upandaji miti. Tarehe 7 Oktoba tutakwenda Wilaya ya Siha na tayari tumezungumza na mhifadhi wa Siha kwa ajili ya kupanda miti,” alisema.
TFS inashiriki maonesho hayo kwa kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa misitu, vivutio vya utalii ikolojia na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.