
21
Nov
Dk Mpango awapa maagizo Ma-RC kupambana na ukame
Mbeya. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, amesema namna ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji ni ushirikiano wa Serikali, wadau na wananchi huku akiwataka wakuu wa mikoa nchini (RC) kusimamia, kutunza na kuhifadhi vyanzo hivyo ili kunusuru maisha ya watu.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Novemba 16, 2022 wakati wa mkutano mkuu wa nane wa mwaka wa bodi za maji za mabonde tisa nchini uliofanyika jijini hapa.
Amesema maeneo ambayo yamevamiwa ikiwamo milima mirefu ya Uruguru mkoani Morogoro wananchi wahamishwe na kutafutiwa sehemu nyingine huku akiwataka wananchi waliofunga utiririshaji maji kwenye bonde la Ihefu wilayani Mbarali kufungua haraka kabla ya Serikali kuchukua hatua.
Amewataka pia wakuu wa mikoa kuzindua program ya upandaji miti ili kufikia lengo la Taifa kupanda miti 2.5 milioni na kuelekeza maeneo yasiyo na vyanzo vya maji kutengeneza mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji.
"Tukichekeana tutaangamiza Taifa, hii kampeni ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya mwanadamu, taasisi zote za serikali, CCM na wadau kama viongozi wa mira na dini, vyombo vya habari hamasisheni utunzaji vyanzo vya maji," amesema Dk Mpango.
Dk Mpango amewataka wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kufuatilia maeneo yenye uhitaji miti kwa kushirikiana na mikoa husika huku akitaka wataalamu wake kushauri miti rafiki wa maji.
"Siyo kila mti ni rafiki wa maji, nyingine inafyonza wataalamu wa TFS wanapaswa kushauri miti mizuri kwa kushirikiana na wananchi ili kutengewa vitalu, hakuna cha tabianchi bali tubadili tabia wananchi," amesema Dk Mpango.
Pia amezitaka wizara za mifugo na uvuvi kukaa meza moja na wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi kujadili muingiliano wa sheria na kuandaa taarifa serikalini ili kuondoa mkanganyiko katika matumizi ya ardhi.
Aidha, amezitaka wizara ya fedha na mipango kujadiliana na wizara ya nishati katika kupunguza bei ya gesi akibainisha kuwa itakuwa changamoto kwa wananchi kuzuiwa kutumia mkaa huku gesi ikiwa juu.
"Unakuta sheria zinagongana huku inasema hivi kule inaeleza hivi hasa kwenye ile mita 60, nendeni mkae pamoja kisha leteni mapendekezo serikalini tulimalize, suala la gesi wizara ya fedha na mipango na nishati wekeni sawa," amesema kiongozi huyo