03
Dec

Serikali Yatoa Wito kwa Wahifadhi Kuongeza Juhudi Katika Kukuza Utalii

Arusha, Desemba 2, 2024 – Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayesimamia utalii, Nkoba E. Mabula, ameendelea kutoa wito kwa wahifadhi na wadau wa utalii nchini kuongeza juhudi katika kukuza na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania. 

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahifadhi wa utalii, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ngorongoro, Jijini Arusha, Ndugu Mabula aliwashukuru wahifadhi kwa kujitolea kwao katika kudumisha vivutio vya utalii na kuongeza tija katika sekta hiyo.

Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), yalilenga kuwajengea uwezo wahifadhi na askari kwa masuala ya kuendeleza mazao ya utalii, ukarimu, masoko, matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wateja, na usimamizi wa mitandao ya kijamii pamoja na uundaji wa maudhui ya kutangaza utalii.

“Sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wa Tanzania, ikichangia 17.2% ya Pato la Taifa na kutoa fursa za ajira,” alisema Ndugu Mabula, akiongeza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika mapato ya nchi, ambayo kwa mwaka 2023 yaliongezeka kwa 31% hadi kufikia dola za Marekani bilioni 3.4. Alisema ongezeko la watalii, kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi 1,808,205 mwaka 2023, ni ushahidi wa mafanikio ya mikakati ya Serikali ya kukuza utalii.

Ndugu Mabula alisisitiza kuwa licha ya vivutio vingi vya utalii vinavyopatikana nchini, kama vile mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro, na Bonde la Ngorongoro, ni muhimu pia kuongeza juhudi katika kuvilinda, kuviendeleza na kutoa huduma bora kwa watalii. Aliongeza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha idadi ya watalii itafikia milioni 5 ifikapo 2025, ikishirikiana na filamu ya “Tanzania, The Royal Tour” ambayo imesaidia kuongeza uhamasishaji wa utalii duniani kote.

“Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inapata mafanikio makubwa na kuvutia wawekezaji,” alisema. Alitolea mfano wa filamu nyingine ya “Amazing Tanzania” ambayo pia inalenga kutangaza vivutio vya utalii.

Aidha, Mabula alizungumzia umuhimu wa utalii wa misitu, akisema kwamba ingawa ni mchanga nchini, kuna fursa kubwa ya kukuza sekta hii kwa ubunifu na ushirikiano wa wadau mbalimbali. Alitoa mfano wa juhudi zinazofanywa katika maeneo ya misitu ya mikoko Tanga, akisema Wizara imetoa shilingi milioni 200 kutekeleza miradi ya utalii huko.

Katika hatua nyingine, Mabula alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu katika kuweka mikakati ya kukuza utalii wa misitu na malikale. Aliwahimiza wahifadhi kutumia mbinu za kisasa za mawasiliano na teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii, huku akiwapongeza waandaaji wa mafunzo haya na kuwataka washiriki kutumia ujuzi watakaoupata kuleta mabadiliko na maendeleo katika maeneo yao.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, alisisitiza umuhimu wa utalii wa misitu na alielezea hatua kubwa zilizochukuliwa na TFS katika kukuza utalii wa mazingira ya asilia. Alitumia fursa hiyo pia kuwashukuru wahusika wote waliochangia mafanikio ya sekta ya utalii nchini.

Kamishna Prof Silayo alisema kuwa, ingawa utalii wa misitu ulianza kutekelezwa kidogo kidogo mwaka 2015, tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) mwaka 2011, sekta hiyo imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. Alisema kuwa utalii wa misitu ni zao jipya liliopewa msukumo mkubwa na limejumuishwa katika Mpango Mkakati wa TFS kwa lengo la kuboresha huduma za utalii katika maeneo ya hifadhi za misitu na vituo vya malikale.

Prof Silayo aliongeza kuwa idadi ya watalii waliotembelea maeneo ya misitu imeongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka 55,427 mwaka 2019 hadi zaidi ya 250,000 mwaka 2024, huku mapato yakiongezeka kutoka milioni 150 hadi zaidi ya bilioni 1.9. Alieleza kuwa mafanikio haya yamechangiwa na juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya utalii na uhamasishaji kupitia filamu kama "Tanzania, The Royal Tour" na "Amazing Tanzania."

Katika maelezo yake, Kamishna Silayo aligusia umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo UNDP/GEF na EAMCEF, katika kutekeleza miradi ya uhifadhi na utalii. Alisisitiza kuwa TFS inaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya utalii, kuanzisha mifumo ya kidigitali ya kufanya miadi, na kuimarisha huduma kwa wateja ili kuendelea kuvutia watalii.

Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dr. Thereza Mugobi, alisisitiza umuhimu wa wahifadhi katika utekelezaji wa Sera na Sheria ya Utalii. Aliwahimiza kuongeza ufanisi katika kazi zao kwa kujua na kutumia vizuri zana na kanuni za utalii, ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

Dr. Mugobi alifafanua kuwa Wizara ina jukumu la kuandaa Sera, Sheria, na Miongozo inayosaidia ukuaji wa sekta ya utalii. Aliwashukuru wahifadhi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza utalii kupitia ubunifu wao na kuanzisha mazao mapya ya utalii. Alisisitiza kwamba mafunzo haya ni muhimu kwa wahifadhi ili kuimarisha sekta ya utalii, ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. 

Mafunzo hayo yaliyohusisha wahifadhi kutoka maeneo mbalimbali ya misitu na vituo vya malikale, yanaonekana kuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza mikakati ya Serikali ya kukuza utalii nchini na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inafaidika na rasilimali za asili zinazopatikana.

Mafunzo haya, yaliyoandaliwa na TFS, ni muhimu kwa wahifadhi na askari, ili kuwajengea uwezo katika kuboresha huduma za utalii na kutoa mchango mkubwa katika kukuza sekta hii muhimu kwa uchumi wa Tanzania.