19
Mar
MAKAMU WA RAIS AONGOZA UPANDAJI MITI SOKOINE, ASISITIZA UTUNZAJI WA MISITU
Na Mwandishi Wetu, Lindi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Balozi Emmanuel Nchimbi, leo Machi 19, 2026 ameongoza zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sokoine mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani sambamba na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti.
Akizungumza mara baada ya kupanda mti, Nchimbi alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa misitu katika kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha ustawi endelevu wa wananchi.
Alibainisha kuwa juhudi za upandaji miti zinapaswa kuambatana na utunzaji wake ili kuhakikisha zinafanikisha lengo la kuongeza uoto wa asili na kuboresha mazingira.
“Ni muhimu kupanda miti, lakini ni muhimu zaidi kuitunza ili iweze kukua na kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla,” alisema.
Aidha, Makamu wa Rais alihimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kitaifa ya upandaji miti, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya “Tanzania ya Kijani” inayolenga kurejesha uoto wa asili nchini.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kunakuwa na elimu ya kutosha kuhusu uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau wa sekta ya mazingira na uhifadhi kutoka ndani na nje ya nchi, yakilenga kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda rasilimali misitu.
Shughuli za maadhimisho hayo zinaendelea kwa siku nne kuanzia Machi 18 hadi Machi 21, 2026, ambapo zinatarajiwa kufikia kilele chake kitaifa mkoani Lindi.