WAZIRI MALIASILI AHIMIZA UHIFADHI WA MISITU NCHINI

Dkt. Pindi Chana akisikiliza maelezo kutoka kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS, Profesa Dos Santos Silayo kuhusu Wakala huo unavyosimamia rasilimali za Misitu na Nyuki.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (pichani juu) akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya kumaliza kuzunguka na kujionea huduma zinazotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Julai 11,2022.
 
Akizungumza na waandishi hao, Mhe. Chana aliipongeza TFS kwa kutenga maeneo maalumu yaliyojikita kutoa elimu na kutoa wito kwa Watanzania wanaotembelea maonesho hayo ya Sabasaba kutokosa kutembelea banda hilo.
 
“Sote leo tumeona masuala ya misitu, hili ni eneo mojawapo ambalo ni muhimu tunalopaswa kulitunza ili tuweze kunufaika sote, tunapotunza misitu, vyanzo vya maji na nishati vinakuwa salama, leo hii tunapoingiza Wanyama tunahatarisha vyanzo vyetu vya maji, nitowe wito kwa wafugaji tuone maeneo yapi yanafaha kufugia na tusifuge maeneo ya hifadhi, 
 
“Habari ya moto katika maeneo ya misitu tunazo sheria na miongozo yakufuata inayoeleza ni namna gani unavyoweza kuanzisha moto pindi unapotaka kuanzisha moto kwa ajili ya kusafisha mashamba bila kusababisha uharibifu wa misitu yetu, ni lazima tutunze misitu,” anasema Mhe. Waziri Chana.
 
Akimkaribisha kwenye Banda la TFS, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema TFS imejipanga kuhakikisha inatumia maonesho hayo kuendelea kukuza na kuboresha uwezo wa kutoa huduma kwa umma.
 
Tangu kuanzishwa kwake, Wakala wa Huduma za Misitu umekuwa ukihakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti na wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki; kuongeza ubora na thamani ya kifedha katika kutoa huduma kwa umma; na umepanua wigo kibiashara na kuongeza maeneo ya uzalishaji miti na mazao ya nyuki ili kukidhi mahitaji halisi, shughuli za uwekezaji, kuboresha njia mbadala za mapato na uboreshaji wa hifadhi za misitu na nyuki kwa ujumla.