Resources » News and Events

TFS YAPEWA TUZO YA MAZINGIRA 2023

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS umepewa tuzo rasmi ya taasisi bora ya Serikali katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti na utunzaji mazingira linakuwa endelevu mwaka 2023. Tulizo Kilaga anaripoti.
 
Tuzo hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Mei 6, 2023 na wakazi wa Watumishi Housing Bunju Mabwepande chini ya mpango wake wa kila mwaka wa Tuzo rasmi ya utunzaji mazingira 'Green Village Estate Mazingira Award’, wakati wa hafla ya kilele cha upandaji miti kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwenye Kijiji hicho.
 
Kamishna wa Uhifadhi TFS, CC Prof. Dos Santos Silayo alikuwa mgeni rasmi na kuwakilishwa na Naibu Kamishna na Mkurugenzi wa Uzalishaji Mbegu Bora za Miti na Vipando TFS, DCC Caroline Malundo aliyepokea tuzo hiyo kwa niaba.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, DCC Malundo amesema anawapongeza wale wote waliotoa wazo la kutoa tuzo ambazo zinatambua mchango wa watu/taasisi waliojitoa kushiriki kutoa mchango wao katika shughuli za uhifadhi wa Mazingira.
 
“Leo hii TFS tumepokea tuzo, tuzo hii imelenga kutupongeza na kutambua juhudi, na mchango wetu kwenye kuimarisha mazingira kwa upandaji wa miti, asante sana!  Tunaahidi kuendelea kuzalisha miche bora ya miti na kushirikiana na wadau wote wa mazingira ambao watakuwa na sisi,” anasema.
 
Reeves Ngalemwa ni Mwenyekiti ‘Kijiji cha Kijani’ Watumishi Housing Bunju Mabwepande amesema wakati taifa likiweka mkazo na kuelekeza nguvu nyingi katika agenda ya upandaji miti kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi, wao waliona kuna haja ya kuanzisha kampeni endelevu ya upandaji miti kuzunguka mazingira ya eneo la Kijiji chao ili pamoja na mambo mengine kupunguza hewa na ukaa katika Jiji la Dares Salaam na kufikia lengo la dunia la kuwa na Majiji ya Kijani (Green Cities).
 
Anaongeza kuwa katika kampeni hio jumla ya miti 1000 imepandwa kwa ufadhili wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)  katika mji wao huku kila mkazi akipewa miti ya kivuli na matunda kupanda katika eneo lake ambapo wamelenga kila nyumba ipande miti 3 ya kivuli na miti 2 ya matunda. 
 
Ngalemwa anasema katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti na utunzaji mazingira linakuwa endelevu wamemaua kuznaisha TUZO rasmi ya utunzaji mazingira iliyopewa jina la ' Green Village Estate Mazingira Award 2023' ambayo mshindi wake atapatikana kila mwaka Kwa kupitia vigezo vitakavyoainishwa na waratibu wa tuzo yaani Kamati ya Afya, Mazingira na Miundo Mbinu ya Kijiji cha Green Village Estate. Mshindi atapewa medali na pesa tasilimu.
 
“Tuzo hii tunataka iwe ya kitaifa na kwa kuanza leo tunaipa TFS kwa kutambua mchango wake katika utunzaji wa mazingira lakini mbeleni tungependa tuibadiri jina kwa kuingiza jina la Prof. Silayo ikiwa ni kutambua mchango wake kwenye uhifadhi, katika hili tunaomba TFS ishirikiane nasi kikamilifu,” anasema Ngalemwa.
 
Watumishi Housing Bunju Mabwepande ni Kijiji chenye idadi ya nyumba 65 ambazo kati ya hizo 57 zinakaliwa na watu na kwa kutambua umuhimu wa suala la umuhimu wa 'ukijani' wanakijiji waliamua kupaita mahali hapo 'Green Village Estate' yaani kijiji cha Kijani kama njia ya kuhamasisha wakazi wake umuhimu na utamaduni wa kuyafanya mazingira yao kuwa kijani.
 
Jumla ya miche ya miti 14 ilipandwa na viongozi mbalimbali katika hafla ya kilele cha upandaji miti kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika makazi ya Watumishi Housing Bunju Mabwepande na maeneo ya Jirani.