TFS KUJA NA MUONGOZO WA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO YA NYUKI

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kitengo cha Rasilimali za Nyuki – Masoko na Ubora wa Mazao ya Nyuki, Mhifadhi Grace Buchukundi akitesti mitambo

Dar es Salaam: Katika kuhakikisha mazao ya nyuki yanayozalishwa nchini yanaendelea kuwa na viwango vya ubora vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS inatarajia kuja na muongozo wa kuongeza thamani ya mazao hayo nchini.
Akizungumza mara baada ya kumaliza mafunzo maalumu ya kuongezaa dhamani ya mazao ya nyuki yaliotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa siku mbili (Juni 3 hadi 4, 2023), Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kitengo cha Rasilimali za Nyuki – Masoko na Ubora wa Mazao ya Nyuki, Mhifadhi Grace Buchukundi anasema lengo la mafunzo hayo yamelenga kuongeza wigo wa uzalishaji wa mazao ya nyuki yalioongezwa thamani.
“Mafunzo haya yamejumuisha wahifadhi wa TFS kutoka kwenye viwanda vyetu vya uzalishaji mazao ya nyuki ambapo lengo letu ni kutengeneza kitabu kitakachotoia muongozo wa kuzalisha bidhaa zilizoongezwa thamani ambayo itatumika katika vituo vyetu vyote,” anasema Mhifadhi huyo.
Aidha, Mhifadhi Buchukundi anasema moja ya mazao bora ya misitu ambayo nchi yetu imejaaliwa ni zao la asali na kwa sasa nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazozalisha asali bora sana duniani na kupitia mafunzo hayo wanakwenda kufungua wigo wa uzalishaji wa mazao ya nyuki yalioongezwa thamani.
Dorothy Narwango ni mmoja kati ya wakufunzi wa mafunzo hayo anasema kupitia mdudu nyuki kuna mazao mengi yanaweza kuzalishwakuongezewa thamani na yakapata soko kubwa kufuatia asali ya Tanzania kuendelea kufanya vizuri katika masoko ya nchi za Umoja wa Ulaya, Uarabuni na kwenye masoko mapya ya Poland na China.
“Nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania kuchangamkia fursa ya kujifunza uzalisha asali pamoja na kuongeza thamani kwa mazao mengine yatokanayo na mdudu nyuki ili kunufaika na uwepo wa masoko,” anasema Narwango.
Mapema wiki hii akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa alisema  katika mwaka 2021/2022 mauzo ya fedha za kigeni kutokana na asali na nta nje ya nchi yalifikia jumla ya Shilingi bilioni 30.58 yaliyotokana na tani 1,562.93 za asali na tani 747.56 za nta.