Resources » News and Events

TFS, Blue Carbon zasaini Hati ya Makubaliano ya Biashara ya Hewa Ukaa

Kampuni ya Blue Carbon chini ya uwenyekiti wa mwanamfame Sheikh Ahmed Dalmook Juma Al Maktoum wa Falme za Kiarabu UAE imetia saini hati ya makubaliano na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika masuala ya kimkakati ya kuongeza uhifadhi na usimamizi wa misitu nchini ili iweze kuchangia kupunguza hewa ukaa.
Hati hiyo ya Makubaliano imesainiwa na Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Prof. Dos Santos Silayo na Mwakilishi wa Kampuni ya Blue Carbon Josiane Sadaka huku wakishuhudiwa na mwanamfalme huyo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo.

Akizungumza mara baada ya utiaji Saini huo uliofanyika jijini Dodoma leo February 6, mwaka huu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana anasema ni muhimu kuendelea kuilinda, kuitunza, kuihifadhi na kuiendeleza misitu yetu kutokana na umuhimu wake kwenye uhai wa mwanadamu.

“Ni wajibu wetu sisi watanzania milioni 61 kuhakikisha kwamba maeneo yetu ya misitu tunayatunza! Hivi sasa kadri tunavyoendelea tunapata mazao mbalimbali ya misitu, hivi sasa kuna biashara kubwa ya hewa ukaa ambapo wizara yangu na VPO tunakwenda kuona namna gani tunaiboresha zaidi, tunazo kanuni, sheria na taratibu tayari chini ya VPO zikieleza biashara hii inafanywa vipi,” Mhe. Balozi Dkt. Pindi .

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo anasema kusainiwa kwa makataba huo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na timu ya wataalamu baada ya mwanamfalme kuonyesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika uhifadhi wa mzingira hususan katika biashara ya hewa ukaa.

Mhe. Dkt. Jafo anasema utiaji wa saihi uliofanyika ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa ndani ambapo baada ya kufanya kazi yao kikamilifu kwa muda mrefu hatimaye pande zote ziliafiki kusaini hati ya makubaliano (MoU).

“Hii ni safari muhimu kwetu kwa sababu kupitia TFS sasa tunakwenda kuhakikisha jambo hili linafanyika ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu tupate kanuni zetu mwezi Oktoba mwaka jana, lakini mwongozo wa mazingira ambao sasa unakwenda kuhakikisha biashara ya hewa ukaa inaanza rasmi nchini kwa lengo la kuhakikicha nchi inajenga uchumi wake lakini kupunguza athari za mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.” Mhe. Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo alisema utiaji saiani huo unaenda kuipa fursa Kampuni ya Blue Carbon kuanza mchakato wa kusajiri miradi yake kwa kuzingatia maelekezo yaliopo katika sheria ya kusimamia na kuratibu biashara ya mkaa ya mwaka 2022.

Kamishna huyo anasema kumekuwa na changamoto nyingi za usimamizi wa misitu katika nchi zinazoendelea licha ya kutakiwa kuhifadhi misitu yake ili kuweka kuchuja hewa ukaa, na sasa biashara ya hewa ukaa inakuja kutoa motisha ya fedha ili iweze kuzisahidia jamii, taasisi na mashirika zinazosimamia misitu ziwezi kusimamia kikamilifu misitu yake. 

“Katika makubariano tuliyofanya leo tutashuhudia kampuni hii ikiwekeza katika miradi ya kimkakati ya kuendeleza rasilimali Misitu na Hifadhi za Wanyamapori, miradi inayokwenda kuanzishwa katika hatua za awali itakuwa katika maeneo yaliyohifadhiwa ya misitu hususan mikoko na wanyamapori lakini baadaye wataongeza maeneo ya hifadhi ya vijiji na kisha watu binafsi,” anasema.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo itasimamia maeneo yaliohifadhi na yale yalioharibiwa ili kuyarejesha kwenye uoto wake wa asili. Tulizo Kilaga anaripoti.