Habari » News and Events

WAZIRI WA MALIASILI DR,DAMAS NDUMBARO AWATAKA WATANZANIA KUJIPANGA KUTUMIA NISHATI YA MKAA MBADALA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dr, Damas Ndumbaro amewataka watanzania kujipanga kutumia Nishati ya  mkaa mbadala ili kuendelea kuilinda misitu isiharibiwe.

Wito huo ameutoa wakati akizindua mkakati wa utekelezaji wa sera ya misitu ya (1998) na utiaji saini wa kanuni za uendelezaji wa Nishati ya mkaa mbadala uliofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma.

Dr,Damas Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea mjini Mkoani humo amesema kuwa watanzania hasa waishio mijini wakitumia mkaa mbadala basi misitu itaendelea kuwa salama na kuvifanya viumbe vinavyoishi kwenye misitu hiyo viendelee kuongezeka kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.

Waziri huyo amesema kuwa hadi sasa hapa Nchini wafanyabiashara 19 wameanzisha viwanda vya kuchakatia Nishati ya mkaa mbadala hivyo kupitia kanuni zilizosainiwa zitawasaidia kupata uwezo wa masoko ndani ya Nchi na Nje,ya Nchi na kuifanya ajira iweze kuongezeka.

Kwa upande wake kamishina wa uhifadhi TFS Profesa Dos Santos Silayo awali amesema kuwa mkaa mbadala unapatikana kwa masalia ya miti na mabaki ya mimea mbalimbali ikiwemo mazao yanayolimwa na Wananchi.

Profesa Silayo amesema kuwa licha ya kulinda misitu lakini bado hata mwananchi ambaye ni mkulima bado atanufaika na mabaki ya mimea ya mazao yake kwa kuwa anaweza akayauza na kisha kumuingizia kipato cha fedha.

Naye mkurugenzi wa misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dr.Ezekiel Mwakalukwa amesema kuwa mkaa ni zao moja wapo linalotokana na mazao ya misitu hivyo utumiaji wa mkaa mbadala utawasaidia  pia Wananchi kutambua faida za matumizi ya mkaa huo.

Utiaji saini huo ambao umeenda sambamba na maadhimisho ya Majimaji selebuka ,umehudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa chama na Serikali pamoja na baadhi ya wakazi wa mjini Songea ambao wengi wao wamedai wamenufaika  na mpango huo wa matumizi ya Nishati ya mkaa mbadala.