SHIGELA: TFS KINARA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS imepongezwa kwa jitihada kubwa inayofanya katika kuhakikisha kuna usimamizi endelevu wa rasilimali za kitaifa za misitu na nyuki ili kuchangia mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Martin Shigela mapema hivi leo wakati akizindua Maonesho ya Tano ya Mfuko na Programu ya Uwezeshaji Wananchi kiuchumi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Mkoani Morogoro. 

“TFS mnafanya kazi kubwa sana katika kuwezesha Wananchi kiuchumi kupitia Uhifadhi shirikishi wa Rasilimali za Misitu, niwaambie tu, nyie hapa ni maarufu, hongereni sana, " Mhe Shigela anasema.

Mhe Paskali Kihanga Meya wa Manispaa ya Morogoro na mfanyabiashara wa mazao ya misitu anasema "Nawapongeza sana TFS kwa kuwepo hapa, bahati nzuri mimi nafahamu umuhimu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia hii sekta ya Misitu ambapo kwa kiasi kikubwa mimi binafsi imeninufaisha sana."

Katika Maonesho hayo yatakayodumu kwa siku nane (Mei 8-14, 2022), TFS inashiriki kutoa elimu ya uhifadhi wa Rasilimali za Misitu na Nyuki pamoja na Utalii Ikolojia ambapo kupitia shughuli hizo imekuwa ikiwezesha Wananchi kiuchumi lengo likiwa nikuongeza tija katika Uhifadhi wa Misitu na Nyuki. 

Awali uzinduzi wa maonesho hayo ulitarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt Ashatu Kijaji ambaye kutokana na wingi wa majukumu aliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Taasisi mbalimbali zimejitokeza katika maonesho hayo.