Habari » News and Events

MHESHIMIWA ZUNGU AFUNGUA MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU USIMAMIZI WA MISITU YA ASILI NCHINI

Bungeni -Dodoma 18 Aprili,2020
 
Wabunge wanaounda Chama cha Wabunge Marafiki wa Mazingira (TAPAFE) wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo wabunge juu ya usimamizi bora wa misitu ya asili iliyomo nchini.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mgeni rasmi ambaye ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Mheshimiwa Mussa Zungu alisema kutokana na kutoweka kwa kasi kwa misitu mingi ya asili, Wizara yake inalo jukumu kubwa kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa kwa kushirikiana na wananchi.

Aidha, Mheshimiwa Zungu alitoa wito kwa wananchi kujikita kwenye matumizi ya nishati mbadala ikiwemo Gesi na Makaa ya mawe ili kukabiliana na upotevu mkubwa wa misitu ya asili na kuepusha uchafuzi wa mazingira unaotokana na hewa ukaa ambayo huzalishwa na kuni na mkaa.

Alisema “pamoja na juhudi zote zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano, Wadau wa maendeleo pamoja na Sekta binafsi, wananchi tuna wajibu wa kushirikiana na wadau hawa ili kukomesha uharibifu wa misitu kwa kujikita kwenye matumizi ya nishati mbadala”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wabunge wanaounda Chama cha Wabunge Marafiki wa Mazingira (TAPAFE) Mheshimiwa Jitu Soni alimhakikishia Mheshimiwa Waziri kuwa Chama hicho kiko tayari kusaidiana na Serikali kutoa elimu sehemu mbalimbali nchini juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu.  

Aidha,Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS),Prof.Dos Santos Silayo alisema takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inapoteza mapato ya shilingi bilioni 200 kila mwaka kutokana na kukosekana kwa usimamizi wa misitu iliyo chini ya mamlaka za vijiji huku hekta laki nne (4) za misitu zikitoweka Kila mwaka.

Naye mtaalam mwezeshaji kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Ndg. Charles Meshack alisema, kati ya hekta milioni 22 za ardhi zilizoko chini ya Vijiji ni hekta milioni 2 pekee ndizo zinazohifadhiwa na mamlaka za Serikali na hivyo kufanya sehemu kubwa ya ardhi ya Vijiji kuwa hatarini kuharibiwa.

Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira yalifanyika kwenye Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma.