Kuhusu Wakala

Naibu Waziri aitaka TFS kufanya kazi kwa bidii na weledi

Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu  za utumishi wa Umma ili kuleta ufanisi  wakati wanapotekeleza majukumu yao ya uhifadhi.

Rai hiyo imetolewa jana  na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakati alipowatembelea jana watumishi wa TFS kanda ya Kusini kwa ajili ya kuzungumza nao ikiwa ni muendelezo ya ziara yake ya kikazi ya  siku mbili mkoani Mtwara kwa ajili ya kushughulikia changamoto za Maliasili, Malikale na Uendelezaji Utalii

Amewataka kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu na yeyote atakayetuhumiwa kupokea rushwa hata kama haijathibitika kupokea  rushwa hiyo atashughulikiwa ipasavyo.

Aliongeza kuwa endapo watumishi hao wataweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo hakuna kiongozi yeyote watakayewasumbuana naye

‘’Tunataka mfanye kazi zenu za uhifadhi  kwa weledi wa hali ya juu na mkifanya vizuri basi nitakuwa nimefanya mimi na mkifanya vibaya nitakuwa nimefanya mimi, hivyo sitokubali mniharibie’’ alisisitiza Naibu Waziri Hasunga.

Aidha, Amewataka wafanye kazi kwa kushirikiana na jamii kwa vile hakuna shughuli yeyote itakayofanikiwa endapo wananchi wataachwa nyuma kwenye uhifadhi.