Habari » News and Events

PROF. SILAYO AWATAKA WALIOVAMIA MISITU HANDENI, KILINDI TANGA KUONDOA

SERIKALI imetaka wananchi wote waliovamia hifadhi za misitu wilayani Handeni na Kilindi mkoani Tanga kuondoka mara moja na kutangaza kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaokahidi agizo hilo huku ikieleza kujipanga kuweka mikakati kuimarisha ulinzi sambamba na kufungua fursa za uchumi kwa wananchi.

Akizungumza jana Februari 28,2023 Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo akiwa ziarani Wilayani Handeni mkoani Tanga na kukutana na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Msomi Mhe. Albert Msando kujadili namna wanavyoweza kushirikiana kuhakikisha rasilimali misitu za wilaya hiyo zinaendelea kuwa endelevu.

Prof. Silayo alisema wilaya ya Handeni kama ilivyo wilaya nyingi nchini wananchi wake wanajishughuliza na shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo na ufugaji ambazo katika utekelezaji wake hujikuta wamevamia maeneo yaliyohifadhiwa.

“NI wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha kwamba maenoe haya yaliohifadhiwa yanaendelea kuhifadhiwa na yanakuwa salama ndio mana leo nimefika hapa kuonana na viongozi wa wilaya hiii kuona ni hatua gani tuchukue katika maeneo yalivamiwa, 

“mfano msitu wa hifadhi wa Bondo uliopo wilayani Handeni na Kilindi pamoja na msitu wa Gendagenda imevamiwa kwa hiyo ni wajibu wetu kuhakikisha wavamizi hawa wanaondoka! Ni maelekezo ya viongozi ni maelekezo ya sheria kwa hiyo ni lazima waliovamia waondoke kabla hatujawaondoa kwa namna yoyote,” anasema.
Sambamba na mikakati hiyo Kamishna huyo anasema jambo linguine walilojadili nikuhakikisha misitu wanayoisimamia inatoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi kama vile ufugaji nyuki ambao utachochea uhifadhi na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Amesisitiza kuwa zoezi hilo litahusisha pia maeneo yaliohifadhiwa kwa ajili ya vyanzo vya maji ambayo kwa bahati mbaya wananchi wameyavamia na kufanya shughuli zisizoruhusiwa. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Msomi Mhe. Albert Msando, ameishukuru TFS kwa utayari wao wa kushirikiana na ofisi nyingine kuangalia ni namna gani rasilimali misitu zinaweza kulindwa na kuhifadhiwa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwe ni pamoja na kuwaonyesha fursa za kiuchumi kama vile ufugaji nyuki wananchi.

“TFS kupitia kwa Kamsishna wa Uhifadhi leo tumeweza kuzungumza na kuafikiana kwamba katika maeneo yote yaliotengwa kwa ajili ya hifadhi ya misitu kwenye Kijiji cha Msomera yaende kutumika katika shughuli za ufugaji nyuki tukiamini ni shughuli ya kiuchumi itakayowaokoa endapo itatokea ufugaji au kilimo kimeyumba,” anasema na kuongeza kuwa Wilaya yake itatoa ushirikiano wote kuhakikisha misitu inahifadhiwa.