Naibu Waziri Mkuu ataka ushirikishwaji wa Wananchi msitu wa hifadhi Kigosi

Geita.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Doto Mashaka Biteko ametoa maelekezo hayo tarehe 06/06/2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Bukombe ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Dkt Biteko ameeleza umhimu wa TFS kuwashirikisha wananchi katika kulinda msitu wa Kigosi huku akiwataka wananchi wa wilaya ya Bukombe kufuata utaratibu kila wanapotaka kuingia kwenye hifadhi hiyo.

"Hili la msitu wa Kigosi,niwaambie ukweli na ndiyo maana nimekuja na Kamishna wa TFS, kwenye msitu ule kuhusu kufuga nyuki tulifaanikiwa, lakini kwa shughuli zingine inabidi kuwa na subira.Serikali ipo itatoa utaratibu wa hizo shughuli zingine kwa hiyo TFS muwe rafiki washirikisheni wananchi na nyie wananchi mfuate utaratibu msichokozane"Mhe Dkt Biteko.

Aidha Dkt Biteko ametaka watendaji wa TFS kuwa wema katika kutekeleza majukumu ya uhifadhi huku akitolea mfano wa wema wa Kamanda wa TFS kanda ya ziwa Bakari Mohamed ambaye awali alipongezwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Ndg Nicholaus Kasendamila kwa utendaji wake mwema.

Katika mkutano huo Kamishna wa uhifadhi ameambatana na wasaidizi wake kutoka TFS makao makuu na kanda ya ziwa ambapo amepokea maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na kuahidi kuyafanyia kazi.

Viongozi wengine walioshiriki mkutano  huo ni Mhe Festo Dugange Naibu Waziri OR TAMISEMI, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martin Shigela,wakuu wa wilaya Bukombe na Mbogwe pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi.