Habari » News and Events

TFS YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KWA SHULE ZA MSINGI MBILI

Tunduma – Songwe: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS umekabidhi Kompyuta 34 na Meza 20 na viti 40 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 40 kwa shule mbili za msingi za Halmashauri ya mji wa Tunduma mkoani Songwe ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga na kuboresha miundombinu ya madarasa nchini.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya TEHAMA Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo mwishoni mwa wiki (Januari 20, 2022) anasema ili uweze kufikisha elimu ya uhifadhi kwa haraka kwa mtu yoyote TEHAMA haiepukiki na kwa sababu hiyo wameamua kuwekeza katika elimu ya awali ili vijana watakaonufaika wakawe mabalozi wazuri wa uhifadhi.

“Leo tumewafikia wanafunzi kwa TEHAMA kwa kugawa Kompyuta 17, Meza 10 na viti 20 kwa Shule ya Msingi Msinde na kugawa idadi hiyo hiyo kwa Shule ya Msingi Tunduma TC yenye mchepuo wa kiingereza, msaada huu ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan lakini pia kuwekeza katika uhifadhi wa nchi ili uweze kuwa endelevu,”

“Sote tunajua Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha wananchi wake wanapata elimu bora na sahihi, nasi TFS tunaungana na mama kuwafikia wahifadhi wetu wa sasa na baadaye kwa kuwapatia kompyuta za kujifunzia, lakini pia meza na madawati kwa kutambua TEHAMA ndio dunia ilipo na inakoelekea,” anasema Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Silayo.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya mji wa Tunduma  Wilson Mtafya alishukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa msaada huo utakaoziwezesha shule hizo mbili nufaika angalau kufikia malengo ya sayansi na teknolojia.

“Serikali yetu imefanya kazi kubwa kuhakikisha Watoto wetu wanasoma kwenye mazingira mazuri lakini kuna changamoto bado, halmashauri yake ina jumla ya shule 49 za elimu ya msingi na shule 16 za elimu ya sekondari ambapo zote zinahitaji angalau kupata kompyuta kumi kila moja kwa ajili ya elimu kwa vitendo, tunamshukuru sana Kamishna Prof. Dos Santos Silayo kwa msaada wake, tunaomba wadau wengine watushike mkono katika hili, “ anasema afisa elimu huyo.

Nicholaus Mtindya ni Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Tunduma TC anasema katika kizazi cha sasa na kijacho TEHAMA ni kila kitu na ina umuhimu mkubwa katika uhifadhi na hivyo kuwezeshwa kuwa na kituo cha TEHAMA kitawarahisishia upatikanaji wa huduma za elimu.

Kwa upande wake Bi. Tutindanga Mwakibete, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mtindwe anasema komputa hizo zitawasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi lakini pia kuongeza ujuzi na ufanisi katika matumizi ya TEHAMA.

Caption: Kutoka kushoto ni Nicholaus Mtindya ni Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Tunduma TC na Bi. Tutindanga Mwakibete, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mtindwe (wa kwanza Julia wakipokea  moja kati ya Kompyuta wailizokabidhiwa na Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo mwshoni Mwalimu alipokuwa kwenye ziara ya Kijazi katika Halmashauri ya mji wa Tunduma mkoani Songwe.