Habari » News and Events

RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AZINDUA SHAMBA LA MITI SILAYO MKOANI GEITA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiwa na viongozi wengine akizindua rasmi Shamba la Miti SilayoRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiwa na viongozi wengine akizindua rasmi Shamba la Miti Silayo
Kamishna wa Uhifadhi - TFS, Prof. Dos Santos Silayo akipiga saluti mara baada ya Rais kutamka kuwa shamba la Miti Chato lililopo Butengo Chato mkoani Geita litakwenda kuitwa jina lake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 27 Januari, 2021 amezindua Shamba la Miti lililopo katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita na kuagiza shamba hilo liitwe Shamba na Miti Silayo ikiwa ni kutambua jitihada za Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania – TFS, Prof. Dos Santos Silayo katika uhifadhi nchini.

Shamba hilo lenye ukubwa wa Hekta 70,000 limeanzishwa mwaka wa fedha 2017/2018 ikiwa ni jitahada za TFS kuitikia wito uliotolewa na Mhe. Rais Magufuli wa kuitaka wakala hiyo kuongeza malighafi zitokanazo na misitu ambapo iliamua kubadili lililokuwa Msitu wa Hifadhi wa Biharamulo - Kahama kuwa shamba la miti baada ya msitu huo kuharibiwa vibaya kutokana na kuvamiwa na wananchi waliokuwa wakiendesha shughuli mbalimbali zisizo za uhifadhi.

Shamba la Miti Silayo linakuwa shamba la pili kwa ukubwa hapa nchini likitanguliwa na Shamba la Miti la Sao Hill lililopo Mkoani Iringa lenye ukubwa wa zaidi ya Hekta 135,903, na linafanya jumla ya idadi ya mashamba ya miti ya Serikali hapa nchini kufikia 23 yenye ukubwa wa hekta 500,000.

Kamishna wa Uhifadhi Prof. Silayo amesema tangu kuanziswa kwake miaka 4 iliyopita shamba hilo limepandwa jumla ya miche 7,449,255 kwenye hekta 2,682 sawa na ekari 6,705 na kwamba shamba hilo  limetoa ajira 800 kwa wananchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuandika historia ya kuwa Rais wa Kwanza kuzindua shamba la miti, na ameeleza kuwa sekta ya misitu ambayo katika mwaka uliopita ilichangia shilingi Bilioni 130 katika pato la Taifa na shilingi Bilioni 373 katika miaka 3 iliyopita imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua kipato cha wananchi akitolea mfano wa halmashauri ya Wilaya ya Mafinga ambayo mwaka jana ilijipatia shilingi Bilioni 1.3 kutokana na misitu.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TFS kwa jitihada kubwa za upandaji miti katika misitu na mashamba mbalimbali hapa nchini na amesema ameamua lililokuwa Shamba la Miti Chato liitwe Shamba la Miti Silayo kwa sababu amejionea jitihada kubwa zilizofanywa na Prof. Silayo katika kulinusuru lililokuwa pori la Biharamuro/Kahama kwa kulifanya shamba la miti ambalo licha ya kuhifadhi mazingira, kuondoa hewa ukaa, kuzalisha malighafi za misitu na kuhifadhi maji litasaidia kuinua maisha ya wananchi bila kuwabagua kwa elimu zao.

Mhe. Rais Magufuli ameitaka TFS kuongeza kasi ya upandaji wa miti ili hekta zote 69,000 za shamba hilo zipandwe, kuweka mikakati mizuri ya uhifadhi wa shamba hilo na kusimamia vizuri rasilimali ya misitu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuhakikisha misitu inainufaisha nchi badala ya kuwanufaisha watu wachache ambao wanasafirisha magogo kwenda nje ya nchi badala ya kusafirisha mazao ya misitu yaliyoongezwa thamani zikiwemo samani.

Ameiagiza TFS na wadau wengine zikiwemo wizara na taasisi za Serikali kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana wa Tanzania kunufaika na mazao ya misitu wakiwemo mafundi seremala pamoja na kuandaa miundombinu ya uchakataji wa mazao ya misitu vikiwemo viwanda vya mbao badala ya kusubiri mpaka uvunaji uanze.

Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wananchi kwa kuridhia eneo hilo kuanzishwa shamba la miti na ameziagiza halmashauri na taasisi mbalimbali nchini kuhimiza upandaji wa miti katika maeneo yao.