Habari » News and Events

MITI YA MISAJI KUIINGIZIA SERIKALI SHILINGI 2.9 BILIONI

MMOJA WA WANUNUZI WA TEAK AKIPIMA GOGO LA MTI ALIOVUNA KUTOKA KWENYE SHAMBA LA MTIBWA

MUHEZA – TANGA: Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 2,933,266,522.26 za kitanzania baada ya kuuza jumla ya meta za ujazo 4,465.735 m3 za miti ya misaji katika Shamba ya Miti Mtibwa - Morogoro na Longuza mkoani Tanga.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mnada uliofanyika katika shamba la miti Mtibwa mapema hivi leo, mwenyekiti wa kamati ya mnada, Afisa Misitu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Seleboni J. Mushi alisema kamati yake imefanya minada miwili na kufanikiwa kuuza mazao yote kwa asilimia mia huku wakikusanya maduhuli ya Serikali kwa asilimia 109.

“Tumefanya minada miwili, mnada katika shamba la miti Mtibwa ulifanyika tarehe 21 Januari, 2022 na leo 24 Januari, 2022 tumefanya katika shamba la miti Longuza na kufanikiwa kuuza jumla ya meta za ujazo 4,465.726m3, Mtibwa 1,268.981 na 3,196s.735 Longuza sawa na asilimia 100 ya ujazo tuliotangaza kuuza,

“Mauzo hayo yalitarajiwa kukusanya jumla ya Shilingi 2,690,989,150.00 kwa bei ya kuanzia. Hata hivyo, baada ya minada kufanyika, makusanyo ya maduhuli ya Serikali yalifikia shilingi 2,933,266,522.26 (asilimia 109) kwa mgawanyo wa shilingi 561,851,525.00 kwa Shamba la Miti Mtibwa na Shilingi 2,371,414,997.26 kwa Shamba la Miti Longuza,” alisema Seleboni.

Aidha, amesema mnada huo umehusisha jumla ya vitalu 32 ambapo kati ya hivyo vitalu vitano vilitengwa katika shamba la miti Mtibwa huku Shamba la Miti Longuza likitenga vitalu 27.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Matumizi ya Rasilimali, Salehe Beleko aliwashukuru wadau wote waliojitokeza katika minada hiyo na kuonyesha ushindani huku akiwaasa kushiriki katika mnada wa kielektroniki utakaofanyika tarehe 26 Januari 2022.