Resources » News and Events

Wizara ya maliasili na utalii yazindua namba za kijeshi za magari, mitambo na vyombo vingine

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imezindua rasmi namba za kijeshi zitakazotumika katika magari, mitambo na vyombo vingine vya moto vya Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo jijini Dodoma Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael amesema Jeshi hilo linafahamika kwa kifupi kama Jeshi la Uhifadhi (JU).
Amesema Jeshi hilo linaundwa na taasisi nne za uhifadhi ndani ya wizara ya Maliasili na Utalii ambazo ni Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimmaizi wa Wanayama pori Tanzania (TAWA) na Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS).

“Sababu kubwa ya kuanzishwa kwa Jeshi la uhifadhi ni kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu na zile zinazo ambatana nazo, Hii ni kufuatia kuongezeka kwa ujangiri wa wanyamapori wakubwa hususani tembo na faru na kuongezeka kwa uvunaji haramu wa mazao ya misitu katika kipindi cha miaka ya 2000” amesema Dkt. Michael.

Aidha, amebainisha kuwa  baada ya uzinduzi wa jeshi la uhifadhi mwaka 2018, Wizara imekamilisha maandalizi ya nyenzo na vitendea kazi mbalimbali vitakavyo saidia utekelezaji wa mfumo wa kijeshi.

“Baadhi ya vitendea kazi hivyo ni pamoja na kanuni za jeshi la uhifadhi, vyuo vya kutolea mafunzo kwa maafisa na askari wake pamoja namba maalumu zitakazokuwa zinatumiwa na magari, mitambo na vyombo vingine vya moto vinavyomilikiwa na jeshi la uhifadhi”amesema

Pia, amesema pamoja na uzinduzi wa namba hizo wamepokea magari mapya 15 ya jeshi la uhifadhi yatakayotumiwa na TFS.“Magari ha yayamenunu liwa kwa fedha za Serikali kama sehemu yakuima risha utendaji wa jeshi letu katika kusimamia rasilimali za misitu na nyuki, magari haya yatagawanywa kwa matumizi katika wilaya za Mlele, Mpanda, Songea, Tunduru, Longido, Rombo, Serengeti, Manyoni, Bahi, Mvomero, Kibaha, Mufindi na Chunya”alisema
Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo, alisema kuzinduliwa kwa namba hizo kutasaidia kutambulisha magari pamoja vyombo vingine vya moto vinavyotumiwa na jeshi hilo.

Akizungumzia kuhusu magari hayo 15 yaliyokabidhiwa amesema yatakwenda kusaidia kuwezesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo. “Magari haya yatakwenda kusaidia katika kuimarisha ulinzi wa rasimali za misitu nchini katika maeneo mbalimbali”alisema
Kadhalika amesema magari hayo 15 ni sehemu ya yale 34 ambayo yaliyo nunuliwa na serikali mwaka jana na kugharimu takribani Sh.bilioni 5.6.

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilema, amesema magari hayo atasaidia kukabilina na ukataji ovyo wa misitu katika hifadhi mbalimbali za Taifa.

“Misitu ni uhai, katika maeneo mengi nchini misitu imeharibiwa sana magari haya yanakwenda kufanya shughuli ya ulinzi wa misitu pamoja na kukomesha matukio ya ujangiri ili kulinda rasilimali zetu tulizonazo”amesema.