Resources » News and Events

WAZIRI MKUU MSTAAFU MIZENGO PINDA AWATAKA VIONGOZI WA RUVUMA KUHAMASISHA UFUGAJI WA NYUKI

Waziri Mkuu Mstaafu wa Kwanza Kulia, akiwa ameshika Jarida la Ufugaji nyuki, Siku ya ufugaji Nyuki Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika uwanja wa Majimaji Songea Mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya chama na SerikaliWaziri Mkuu Mstaafu wa Kwanza Kulia, akiwa ameshika Jarida la Ufugaji nyuki, Siku ya ufugaji Nyuki Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika uwanja wa Majimaji Songea Mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya chama na Serikali

Ruvuma.
WAZIRI mkuu mstaafu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuhamasisha ufugaji wa nyuki kwa wakazi wa mkoa huo ili waweze kujiongezea uchumi kupitia mazao yanayotokana na Nyuki hao.

 Wito huo ameutoa wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo kwenye siku ya ufugaji Nyuki Duniani ambayo kitaifa imefanyika katika uwanja wa Majimaji Songea Mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya chama na Serikali pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro.

 Pinda ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye siku hiyo ya ufugaji Nyuki amesema kuwa wakazi wa mkoa huo wakihamasiswa kikamilifu namna ya ufugaji Nyuki itawasaidia wakazi hao kujiongezea uchumi wa kifedha kwa kuwa mazao yanayotokana na wadudu hao yamekuwa na thamani kubwa.

Amesema ili kufanikisha zoezi hilo la ufugaji wa nyuki uongozi huo unatakiwa kuunda vikundi mbalimbali vya ufugaji Nyuki kisha vipatiwe elimu ya namna ya kufuga kwa mfumo wa kisasa na mwisho wa siku wanakuwa wafugaji bora wa wadudu hao ambao hutoa mazao ikiwemo zao la asali ambayo ni bora na inapendwa Nchi nyingi.

Aidha Pinda amepongeza kazi inayofanywa na Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS)kwa kulinda mapori mengi Tanzania na kuyafanya yaendelee kuwa na uoto wa asili jambo ambalo litaongeza uzalishaji wa mazao yanayotokana na Nyuki.

 Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa Wizara yake imejipanga vema kuhakikisha elimu inatolewa kwa wafugaji hao na kuwa Wizara  imeanzisha viwanda vikubwa vitano hapa Nchini vinavyosindika mazao yanayotokana na Nyuki.
 
 Dkt Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea mjini amesema kuwa Nyuki ni wadudu wanatakiwa kuheshimiwa licha ya kupata mazao yake lakini bado wanakazi ya kuchavua kwenye mazao mengine na kuyafanya mazao hayo yaweze kuzalisha chakula na kuwafanya binadamu wasife njaa.

Naye mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani humo Pololet Mgema akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge amesema kuwa licha ya kuwepo kwa wafugaji Nyuki  mkoani humo kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya watu kufanya vitendo viovu vya uchomaji wa misitu na kusababisha madhara kwa wafugaji Nyuki.

 Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa sekta hiyo imejipanga vema kuendelea  kuimalisha uhifadhi wa misitu ili iendelee kutoa mazao mbalimbali ikiwemo mazao yanayotokana na ufugaji wa nyuki.

 Siku ya ufugaji wa nyuki Duniani katika Viwanja vya Majimaji Songea imeenda sambamba na tamasha la majimaji selebuka ambalo kilele chake Julai 31 mwaka huu ambapo washindi mbalimbali watajinyakulia zawadi zilizoandaliwa.