Resources » News and Events

WANANCHI WAPEWA WITO KUWEKEZA KWENYE MISITU WA PUGU KAZIMZUMBWI

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akichana mfuko uliowekewa mche wa mti kabla ya kuupanda , leo Machi 6,2021 katika eneo la nje ya geti la Hifadhi ya Msitu Asilia wa Pugu Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe mkoani Pwani.Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akichana mfuko uliowekewa mche wa mti kabla ya kuupanda , leo Machi 6,2021 katika eneo la nje ya geti la Hifadhi ya Msitu Asilia wa Pugu Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa mwito kwa wananchi, wadau na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika misitu ya Serikali ambayo imehifadhiwa na TFS ukiwemo Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi ulioko wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

Aidha katika kuhakikisha uhifadhi wa mazingira pamoja na utalii ikolojia unakuwa endelevu, TFS imekuwa na utaratibu wa kuwa na programu za kutoa elimu kwa watoto ili kutambua mapema kuhusu uhifadhi wa misitu na faida zake, pamoja na kuwahamasisha kupanda miti.

Akizumza leo Machi 6, mwaka 2021 baada ya tukio la upandaji miti lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo lililofanyika katika Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ikiwa ni sehemu ya shughuli zilipo katika Tamasha la Kisarawe Ushoroba Festival Kaimu Meneja Mawasiliano TFS Martha Chassama amesema ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha anakuwa mdau katika eneo la uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha utalii hasa wa kutembelea hifadhi za misitu ya asili.

Kuhusu TFS kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu nchini, amesema mbali ya kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa elimu kwa watoto kwa kutambua watoto ndio wahifadhi wa kesho lakini pia watalii wa kesho.

"Kwa msingi huo ndio maana leo kwenye tukio la upandaji miti watoto nao wameshiriki kikamilifu, wamepanda miti, lakini watoto wameedelea kupewa elimu ya uhifadhi, hivyo sisi TFS kutoa elimu ka watoto wadogo ni jambo muhimu na tunalipa kipaumbele.

"Tunataka mtoto akiendelea kukua anajua umuhimu wa kutunza mazingira, kutunza misitu ya asili, kutunza uhifadhi lakini mtoto awe anapenda kupanda miti ya matunda, asili, miti ya kivuli pamoja na miti yakiimani,"amesisitiza Chassama.

Kuhusu tamasha la Kisarawe Ushoroba Festival, amesema ni tamasha ambalo limesaidia kuendelea kuelezea hifadhi ya msitu wa asili ya Pugu Kazimzumbwi ambao uko chini ya TFS.

"TFS tumetengeza umakini kwa watu wanaoishi maeneo ya msitu Kazimzumbwi, katika masuala ya uhifadhi wananchi wameendelea kuwa na uelewa na tumehamasisha upandaji miti,"amesema na kusisitiza katika msitu huo TFS wanahamasisha wadau kuwekeza kwani kwa mujibu  wa sheria wanalo jukumu la wao kuuendeleza.

Baadhi ya wadau wa mazingira wakipanda miti.

Akizungumzia msitu huo wa Pugu Kazimzumbwi, amesema pamoja na aina nyingine ya utalii, kuna utalii ikolojia ambao ni utalii tulivu na watu wanaweza kwenda katika utalii huo.

"Utalii ikolojia ni utalii ambao unaambatana na utulivu, sio utalii wa kuona wanyama, ni utalii ambao mtu anaweza kufanya tahajudi kwa maana ya kufanya maombi kwa muumba wake.Aidha katika msitu wa utalii ikolojia mtu anaweza kupeleka mgonjwa kwa ajili ya kufanya mazoezi katika eneo ambalo limetulia na halina vurugu,"amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Joketi akipiga kasia katika bwawa la Minaki lililopo ndani ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ulioko wilayani kwake ikiwa. ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kufika na kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.

"Sehemu kama hizi unaweza kumleta mgonjwa ukamtembeza umbali wa kilometa moja, mbili au tatu na hasa kwa wagonjwa waliofanyiwa operesheni,"amesisitiza Chassama huku akiendelea kuhamasiaha wananchi kujenga utamaduni wa kutemebelea msitu huo.

Awali Kamishna wa Uhifadhi Prof. Dos Santos Silayo amefafanua katika misitu huo wa Pugu kuna aina mbalimbali za vivutio vya utalii na vingine hakuna mahali vinakopatikana zaidi ya ndani ya msitu huo tu.

"Kuna miti ya aina mbalimbali, kuna mazingira mazuri lakini pia kuna ndege wadogo ambao wako hapa tu.Aidha kuna ndani ya msitu huu kuna mito yenye chemchem za maji, kwa hiyo tamasha hili la Kisarawe Ushoroba Festival limekuja wakati muafaka na lina faida nyingi.

"Kwa hiyo tamasha hili tumeona tunayo sababu ya kuungana na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha tunashirikiana naye katika kila hatua, na tunaimani kuona likiendelea kuwa endelevu kwa kufanyika kila mwaka,"amesema.

Muonekano wa Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi ulioko wilayani Kisarawe mkoani Pwani ukipigwa picha kwa juu, bwawa linaloonekana ndilo mhe. Joketi alilopo akipiga kasia.