Resources » News and Events

USAFIRISHAJI WA VIUMBE HAI NJE YA NCHI WAWAATHIRI WAFUGAJI MILIMA YA AMANI MUHEZA.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji  ya Umma (PIC), imejia juu katazo la kusafirisha viumbe hai nje ya nchi jambo ambalo  limewaathiri wafugaji wa vipepeo katika milima ya Amani wilayani Muheza Mkoani Tanga.  

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa wilayani Muheza wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Amani ambapo amesema ipo haja ya serikali ipitie sheria hiyo na kuangalia namna ambavyo wananchi waliokuwa wanafuga vipepeo na kuwauza nje nchi kwa ajili ya kujipatia kipato wameathirika.

Wakiwa kwenye hifadhi hiyo wabunge pamoja na mambo mengine wamezungumzia zuio hilo la usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi kitendo ambacho kimewaathiri wazalishaji ambapo wameitaka wizara husika kulifanyia marekebisho jambo hilo. 

"Niseme tu kwamba serikali ilitoa katazo baada kuingia dosari ya kusafirisha viumbe wengine zaidi ya vipepeo, hivyo tunapendekeza ipitie sheria hiyo ili kuendeleza ufugaji wa vipepeo kwa wananchi na kujiongezea vipato vyao," amesema Silaa. 

Kamati hiyo pia ilijionea miradi mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo inayotekelezwa na TFS katika msitu huo.

"Tumejionea mambo mengi tukiwa katika hifadhi hii, aina mbalimbali za miti ambayo inapatikana hapa, ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na njia za watembea kwa miguu na majengo na tumefurahishwa," amesema Silaa.
Sambamba na hayo wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na matumizi ya fedha za Serikali zilizotolewa kwa ajili  ya maboresho ya miundombinu ya barabara na majengo.

Kwa upande wake Kamishna wa wakala wa huduma za misitu Tanzania (TSF) ,Prof Dosantos Silayo amesema suala la ufugaji wa vipepeo kwa wakazi wa eneo la amani wamepokea maelekezo ya Kamati hiyo na kwamba watalifikisha wizarani. 

Prof Silayo amezitaja fursa zinazopatikana katika misitu hiyo kuwa ni utalii wa misitu kilimo cha viungo pamoja na ufugaji wa vipepeo pia tasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wanaishi pembezoni wa misitu hiyo. 

Akizungumzia changamoto ya upungufu wa watumishi pamoja na uwepo wa watumiahi wa kada ya utalii utasaidia kutangaza utalii wa misitu. 

Zuio la kusafirisha viumbe hai lilitolewa na serikali mwaka 2019 na kuwaagiza wasafirishaji wa vipepeo nje ya nchi na baadae kusababisha athari za kibiashara kwa wazalishaji wa vipepeo hao.