Resources » News and Events

Tutailinda Misitu angani na ardhini – Prof. Silayo

Dodoma: Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema usimamizi na ulinzi wa rasilimali za misitu utafanyika kutokea ardhini na ikilazimu angani, ili kuhakikisha inakuwa endelevu kwa ajili ya maisha ya wananchi.
 
Profesa Silayo aliyasema hayo baada ya kumaliza doria ya anga aliyoifanya kuzunguka Msitu wa Hifadhi Chenene uliopo Bahi ambapo aliambatana na uongozi wa Wilaya ya Bahi, watendaji wa vijiji na kata zinazozunguka msitu huo.
 
Kamishna huyo alisema msitu huo ni miongoni mwa misitu 20 ya Mkoa wa Dodoma ambao umekuwa ukiathiriwa kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwamo uchomaji wa mkaa, ufugaji wa mifugo na makazi.
 
Alisema Wakala wa Huduma za Misitu umejipanga kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaofanya shughuli hizo kinyume cha sheria ndani ya msitu huo ukishirikiana na viongozi wa vijiji na kata ili kuhakikisha kwamba wanaondoka.
 
Profesa Silayo alisema uamuzi wa kufanya doria hiyo wakiambatana na viongozi wa vijiji na kata ulilenga kuwafanya pamoja kujionea hali halisi ya uharibifu ili hatua zikianza kuchukuliwa wawe kitu kimoja katika kuhakikisha wanafanikiwa.
 
“Tumefanya doria hii ya anga kwa sababu ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa rasilimali hii ya misitu tunaisimamia kutokea ardhini na ikiwezekana angani... msitu huu (wa Hifadhi wa Chenene) unategemewa kutokana na kuwa mkubwa katika mkoa huu Dodoma na dakio la maji yanayoenda kutokea chanzo cha maji cha Mzakwe kwa ajili ya mji wa Dodoma,” alisema Profesa Silayo.


 
Kamishna huyo alieleza pia mikakati mbalimbali ya uhifadhi wanazochukua ikiwamo upandaji miti katika mji wa Dodoma – kazi ambayo inaendelea vizuri ukiwa ni mpango wa kuifanya kuwa ya kijani.
 
“Mnafahamu kuwa tayari Dodoma tumefanya kazi ya kupanda miti na kazi inaendelea vizuri, lakini kazi kubwa ni kuhakikisha misitu yetu inakuwa salama na katika hali nzuri,” alisema.
 
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda alisema katika ziara waliyowahi kuifanya kipindi cha nyuma walitembelea eneo dogo, hivyo katika doria ya anga wamegundua kwamba kuna uharibifu mkubwa umefanyika katika msimu huo.
 
“Tumeona uharibifu mkubwa, kuna uchomaji wa mkaa, ufugaji wa mifugo na makazi… kuna mahema mle ndani. Hivyo kama viongozi wa wilaya tunajipanga kuchukua hatua maana inawezekana hata waharifu wakajificha humo ndani,” alisema.
 
Aliongeza kuwa, kwa ukubwa wa msitu huo na manufaa unaoyatoa kunyonya hewa nyingi ya ukaa mkoani Dodoma, wao kama viongozi wa wilaya hawatakubali kuuona ukifanyiwa uharibifu wa aina yoyote.
 
Diwani wa Kata ya Zanka, Deo Jeuza alisema msitu huo umekumbwa na uharibifu na kuwataka wananchi wanaojihusisha na shughuli za kibinadamu eneo hilo kuacha na kuondo