Resources » News and Events

TFS YACHANGIA ZAIDI YA MILIONI 20 HARAMBEE YA KUBORESHA HUDUMA ZA MAKUMBUSHO YA MAJIMAJI SONGEA

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Damas Ndumbaro Kushoto akiwa na Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo wakati wa Harambee ya uchangiaji wa ukarabati wa Makumbusho ya Maji Maji Mjini SongeaWaziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Damas Ndumbaro Kushoto akiwa na Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo wakati wa Harambee ya uchangiaji wa ukarabati wa Makumbusho ya Maji Maji Mjini Songea

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana imechangia zaidi ya milioni 20 kwenye harambee ya kuchangia uboreshaji wa huduma za Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi na hasa uhifadhi wenye kuleta tija kwenye uchumi wa nchi, Kamishna wa Uhifadhi  TFS Prof. Dos Santos Silayo alitoa ahadi ya kuchangia shilingi milioni 20 lakini pia alishiriki mnada na kununua fulana na vikombe kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas D. Ndumbaro alieongoza harambee hiyo ambayo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Chifu wa kabila la Wangoni, Chifu Emmanuel Zulu Mbano na mkuu wa wilaya ya Songea na wadau mbalimbali wa malikale, Makumbusho ikiwemo taasisi za Serikali na taasisi binafsi na mtu mmoja mmoja.

Nimenunua fulana kwa ajili yangu na nyingine kwa ajili ya wadau wangu, na hata hivi vikombe vingine nitampa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Freddy Manongi yeye hajabahatika kufika hapa leo ila amewakilishwa, haya yote nimefanya kwa kutambua umuhimu wa mchango wa uhifadhi katika kukuza uchumi wa nchi na umuhimu wa wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kuona moja kwa moja manufaa yake,” Prof. Dos Santos


 
Katika Harambee hiyo inayoendelea kwa njia ya mtandao wa makumbusho, https://www.nmt.go.tz jumla ya shilingi milioni 200 zinakusudiwa kukusanywa ili kuwezesha koboresha miundombinu ua uhifadhi na utalii wa Makumbusho ya Kitaifa ya Majimaji Songea ikiwemo ujenzi wa maduka na banda la wajasiliamali yatakayotoa fursa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Ruvuma na ukarabati wa uzio.

“Asante sana Prof. Silayo na wengine wote mliochangia, nyinyi mmekuwa sehemu ya historia ya makumbusho haya! Fedha hizi zitakwenda kuboresha miundombinu ya Makumbusho ya Kitaifa ya Majimaji zina maana kubwa sana kwetu, zinakwenda kuongeza ajira hususan kwa vijana kwa kuongeza huduma za michezo ya watoto na maeneo ya kupumzikia huku ikiongeza thamani na mvuto wa makumbusho haya,” alisema Dkt. Ndumaro.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga aliwashukuru wale wote waliojitoa kuhakikisha wanachangia na kuwaomba wadau walioshindwa kufika kwenye harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbu wa Manispaa ya Wilaya ya Songea kuendelea kuchangia kiasi chochote cha fedha au kuchangia namna kwa namna yoyote kuboresha makumbusho hiyo kupitia njia ya mtandao ama kufika kwenye makumbusho ya Majimaji ama yoyote ile ya hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine taasisi mbalimbali zilichangia ikiwemo Tawa na TaFF waliochangia shillingi milioni kumi kila mmoja, TAWIRI na TAFORI walichangia milioni tano kila mmoja.