Resources » News and Events

TARATIBU ZA KUSAFIRISHA MAZAO YA MISITU NA NYUKI NJE YA NCHI

Moja kati ya magari yanayohamisha magogo kutoka Shamba la Miti la Serikali Sao Hill Mafinga mkoani Iringa kwenda kwenye viwanda vya wavunaji tayari kwa kuchakata magogo hayo na kupata mbao ambazo huuzwa kwenye soko la ndani na nje ya nchi.Moja kati ya magari yanayohamisha magogo kutoka Shamba la Miti la Serikali Sao Hill Mafinga mkoani Iringa kwenda kwenye viwanda vya wavunaji tayari kwa kuchakata magogo hayo na kupata mbao ambazo huuzwa kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

Mazao ya misitu ni kati ya mazao yanayozalishwa nchini na kuuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Ili kuhakikisha kuwa biashara na usafirishaji wa mazao ya misitu inafanyika kwa njia halali, Serikali imeweka Sheria, Kanuni na Taratibu zinazopaswa kufuatwa na wafanyabiashara na wasafirishaji wote wa mazao hayo ndani na nje ya nchi. Zifuatazo ni taratibu za kuzingatia katika usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi.

1.    MAZAO YANAYORUHUSIWA

  • Vinyago na sanaa

Vinyago ni moja ya biashara zinazochangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini na hata kutangaza utamaduni wa Tanzania kitaifa na kimataifa. Ni biashara inasaidia kuzalisha ajira, kuendeleza teknolojia ya uchongaji, kuongeza pato la taifa na kuenzi na kuendeleza sanaa za maonyesho.

Bidhaa zingine ni:-

  • Mafuta ya msandali
  • Gundi ya miti
  • Chavua
  • Mbao 
  • Magome ya miti

2.    TARATIBU ZA USAFIRISHAJI WA MAZAO YA MISITU NJE YA NCHI

Usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi utafanyika baada ya kukamilisha kazi ya upangaji wa madaraja kwa mazao kama mbao, ukaguzi (inspection) na kupata Hati ya kuruhusu usafirishaji nje ya nchi (Export certificate). 

2.1         Usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi kwa lengo la matumizi binafsi au zawadi (consignment whose value is less or equal to USD 300.00 will be considered as non-commercial consignment).

2.1.1    Upangaji wa madaraja ya mbao hufanyika kwa gharama ya TZS 11,000 kwa mzigo usiozidi meta za ujazo 20.

2.1.2    Hati ya ukaguzi

a)    Kwa mzigo wa vinyago vyenye uzito wa kilo 0 hadi 15 HAKUNA malipo yanayohitajika kwa ajili ya utoaji wa hati ya ukaguzi; Hati itatolewa BURE.

b)    Kwa mzigo wa vinyago vyenye uzito wa zaidi ya kilo 15 YATAHITAJIKA malipo ya TZS 8,700.00 kwa kila mzigo usiozidi tani 20 kwa ajili ya utoaji wa hati ya ukaguzi.

Pichani ni Kamishna wa Uhifadhi-TFS, Prof. Dos Santos Silayo akikagua kinyago katika moja ya mabanda ya wajasiriamali wa bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu nchini wanaofanya biashara ya kuuza vinyago na mapambo jijini Dar es salaam waliofika katika Kongamano la Kimataifa la Sayansi Juu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu na Nyuki kwa Maisha Endelevu na Uchumi wa Viwanda linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Februari 23-25, 2021

2.1.3    Cheti cha kusafirisha mazao ya misitu nje ya nchi (Export certificate)

a)    Kwa mzigo wa vinyago vyenye uzito wa kilo 0 hadi 15 HAKUNA malipo yanayohitajika kwa ajili ya utoaji wa Export certificate; Kibali kitatolewa BURE.

b)    Kwa mzigo wa vinyago vyenye uzito wa zaidi ya kilo 15 YATAHITAJIKA malipo ya TZS 11,000.00 kwa kila mzigo usiozidi tani 20 kwa ajili ya utoaji wa Export certificate.

2.2         Usafirishaji wa kibiashara

Usafirishaji utafanyika baada ya kukamilisha yafuatayo:

Ø  Usajili wa kufanya biashara ya mazao ya misitu (vinyago) nje ya nchi. Usajili unafanyika kwa mwaka kwa gharama ya TZS 512,000.00.

Ø  Hati ya ukaguzi kwa gharama ya TZS 153,400 kwa mzigo usizidi tani 20.

Ø  Export certificate kwa gharama ya TZS 150,500 kwa mzigo usiozidi tani 20.

ANGALIZO

Ni vizuri ifahamike kuwa tozo zilizotajwa hapo juu zinatozwa kwa vinyago vyote ambavyo uvunaji wa malighafi iliyotumika kutengenezea vinyago imepatikana kwa kufuata utaratibu, ISIPOKUWA pale itakapobainika kuwa malighafi iliyotumika kutengenezea vinyago hivyo haikupatikana kwa kufuata utaratibu au vinyago hivyo vimenunuliwa katika maduka yasiyosajiliwa/kutambulika na Wakala, mmiliki wa vinyago atapaswa kulipa ada (Jedwali Na. 1) ikiwa ni nyongeza ya malipo tajwa hapo juu.

2         MAZAO YA MISITU YASIYORUHUSIWA KUSAFIRISHWA NJE YA NCHI

Magogo ya miti aina yoyote na umbo lolote, nguzo zisizowekwa dawa, mizizi, mkaa na fito (withies).

3         Mahitaji ya kibali (CITES certificate) kwa mazao (products) zinazotokana na mti wa Mpingo

Katika usafirishaji wa mbao na vinyago vilivyotengenzwa kwa mti wa mpingo kwa malengo yoyote yale (biashara au matumizi binafsi/zawadi), msafirishaji atahijika kuwa na cheti cha CITES. Hili ni takwa la kimataifa kutokana na Tanzania kuridhia makubaliano ya kulinda viumbe (mimea na wanyama) vilivyo hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na mti wa jamii ya mpingo. Cheti cha CITES kinapatikana kwa gharama ya TZS 5,900.00 (TZS 5,000.00 gharama ya kibali na TZS 900.00 ni VAT) kwa kibali. Aidha, hakuna hitaji la cheti cha CITES kwa mzigo wa vinyago vya mpingo vyenye uzito wa kilo 0 hadi 10.

Imetolewa na 

KAMISHNA WA UHIFADHI WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA