Resources » News and Events

Serikali kupata shilingi Bilioni 1.7 kwa kuuza magogo ya Mkurungu

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS inatarajia kuingiza takriban shilingi bilioni 1.7 kufuatia mauzo ya magogo ya Mkurungu (Pterocarpus Tinctorius) kwa njia ya mnada wa kielectronic.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mnada uliofanyika kwa njia ya mtandao leo Aprili 6, 2022 kuanzia saa sita na dakika moja usiku (6:01) hadi saa saba kamili ya mchana (7:00), Afisa Misitu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Seleboni J. Mushi anasema Serikali imefanikiwa kuuza lot 4 za magogo hayo zenye jumla ya meta za ujazo 989.986.

Anasema kupitia mauzo hayo, Serikali inatarajia kukusanya maduhuli ya shilingi 1.686,301,000 kutoka kwa kampuni tatu Dazhong Wood Industry Company Limited, Eat Africa Born Wood Company na Abduk Bruce China Tanzania zilizoshinda.

“Mnada huu umefanyika kwa mafanikio na ushindani ulikuwa mkubwa, kampuni 13 zilijitokeza kushiriki lakini tatu kati ya hizo ndizo zilizofanikiwa kununua lot 4 huku lot 2 zenye jumla ya meta za ujazo 367.04 zikisalia,

“Washindi wote tumeshawapa barua ya ushindi sambamba na hati ya madai ya asilimia 25 wanazopaswa kuzilipa ndani ya masaa 24 baada ya mnada kufungwa huku asilimia 75 zilizobaki wakitakiwa kulipa ndani ya siku 14,” anasema Seleboni.

Aidha, anasema lot mbili zilizosalia ambazo ziko katika makasha yaliyohifadhiwa katika eneo la Bandari Kavu Ubungo jijini Dar es Salaam zitafanyiwa utaratibu wa kuuzwa tena.