ROYAL TOUR KUCHOCHEA UTALII WA MAZINGIRA NCHINI

Arusha. Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS Prof. Dos Santos Silayo amesema kuzinduliwa kwa Royal Tour kutachochea uwekezaji katika misitu na ukuwaji wa utalii wa mzingira nchini.

Ameyasema hayo jana Alhamisi Aprili 28, 2022 jijini Arusha katika uzinduzi wa filamu ya  Royal Tour na kusema kuwa, Tanzania sasa itawavutia wawekezaji na watalii wa kutosha ambao watasaidia kuongezeka kwa pato la Taifa.

"Royal Tour ni tukio muhimu sana na sisi kama TFS tunalichukulia kwa uzito mkubwa kwa sababu ni hatua ambayo mhe.  Rais mwenyewe amechukua jukumu la kuieleza duniani ni nini Tanzania ilichonacho kinachoweza kutoa duniani ili kuvutia uwekezaji na masuala ya utalii, hili lina maana pana sana katika uhifadhi, utalii na uwekezaji,” anasema Kamishna wa Uhifadhi Prof. Silayo.

Anaongeza kuwa, licha ya nchi kujipambanua zaidi kwenye utalii wa wanayamapori na fukwe zilizopo visiwani Zanzibar lakini duniani kuna utalii wa mazingira unaojulikana kama utaliii ikolojia ambao ni maarufu, na hapa nchini tuna fursa ya kuufanya kutokana na kuwa na misitu mikubwa iliyohifadhiwa.

“Hapa Tanzania tuna fursa yakufanya utalii ikolojia, tuna misitu mikubwa iliyotawanyika katika ikolojia mbalimbali na sisi kama TFS tunajipambanua katika zao hili, utalii ikolojia tukionyesha dunia kwamba tunayo misitu ambayo wanaweza kutalii au kuwekeza katika shughuli zinazohusiana na uhifadhi, tunaamini kupitia Royal Tour wigo wa shughuli za misitu utaongezeka,” alisema Kamishna wa Uhifadhi Prof. Silayo

Anaongeza kuwa maandalizi ya kupokea wageni yameshafanyika kupitia fedha walizopewa na mhe. Rais na kuwekezwa kwenye kuboresha miundombinu katika Misitu ya Hifadhi ili kuweka mazingira wezeshi kwa watalii na wawekezaji.