Resources » News and Events

Mwenyekiti PIC aipongeza TFS kwa usimamizi mzuri wa fedha za MiradI

Akizungumza katika kikao Maalumu kilichofanyika tarehe 20/03/2022 baada ya kukagua miradi inayotekelezwa na TFS katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira asilia Amani uliopo Wilayani Mheza Mkoani Tanga,Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma Mheshimiwa Jerry Slaa Mb ameipongeza TFS kwa kusimamia vizuri fedha zinazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.

*"Kwa namna ya pekee kabisa nawapongeza TFS , ukiangalia kazi iliyofanyika na fedha iliyotumika unaona kabisa thamani yake, nawapongeza kwa dhati kabisa na sisi tutakapopata wasaa mzuri tutaisemea TFS kama mfano"* Mh Slaa.

Aidha Mwenyekiti huyo wa PIC amekiri kuridhika na mwenendo wa utendaji wa kampuni zinazofanya ujenzi wa miradi katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Amani na kuzitaka zihakikshe miradi inakamilika ifikapo Aprili kama ilivyobainishwa kwenye mikataba.

"Pamoja na kuwapongeza TFS, tumeridhika pia na kampuni za serikali zinazofanya kazi hapa, TFS mnafanya kazi na TARURA hapa, hata Kampuni ya Sayaka Civil Work nawapongeza pia, niwatake tu mhakikishe miradi hii inakamilika ndani ya muda uliopangwa." Mh Slaa.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya TFS Mhandisi Enock Nyanda amekiri kupokea pongezi zilizotolewa na Mwenyekiti na Wajumbe wa PIC na kuahidi kufanyia kazi maagizo nane yaliyotolewa na Kamati hiyo kwa niaba ya Bodi na Wizara.

"Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, niseme tu kwa niaba ya Bodi na Wizara tunapokea maagizo nane ya Kamati yako na tunaahidi kuyafanyia kazi namna ipasavyo" Mhandisi Nyanda.

Awali akitoa taarifa fupi ya utangulizi, Kamishna wa Uhifadhi TFS Profesa Dos Santos Silayo amewaeleza wajumbe wa PIC mwenendo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na TFS Katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Amani ukiwemo Mradi wa Lango kuu unagharimu takribani milioni 207 kutoka fedha za Mradi wa kupunguhza athari za UVIKO 19, mradi wa ujenzi wa kilomita kumi za barabara kwa kuwango cha lami unaogharimu takribani milioni 230 kutoka fedha za Mradi wa kupunguza athari za UVIKO 19 na Mradi wa ukarabati wai Nyumba ya wageni unaogharimu takribani milioni 341 kutoka bajeti kuu ya TFS.

TFS imewekeza jumla ya shilingi bilioni moja nukta mbili katika kutekeleza miradi mbalimbali katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Amani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo takribani milioni 500 zimetokana na Fedha za Mradi wa kupunguza athari za UVIKO 19.