MAKAMU wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua Mpango wa Kwanza wa Ufugaji Nyuki pamoja na Mpango wa Tatu wa Utafiti wa Misitu ikiwa ni mkakati katika kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya misitu na nyuki.
Mbali ya kuzindua mipango hiyo, Makamu wa Rais ametoa maelekezo na maagizo kwa wadau wa sekta ya misitu na nyuki huku akitaka tafiti ambazo zinafanywa na watalaamu katika sekta hiyo ziende kwa wadau badala ya kufungiwa makabatini.
Akizungumza leo Februari 23,2021, kwa niaba ya Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, wakati akizundua Kongamano la Kimataifa la sayansi kuhusu mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki kwa maisha endelevu na uchumi wa viwanda, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt.Damas Ndimbaro amesema amewaambia wadau hao yeye amemwakilisha Makamu wa Rais ambaye ndiye mgeni rasmi,hivyo atasoma hotuba kama ilivyo.
"Kabla ya kuanza kusoma hotuba naomba nieleze, nimekuja hapa kumwakilisha Makamu wa Rais, hotuba ambayo nitasoma hapa ni ya Makamu wa Rais si yangu, hivyo maagizo na maelekezo ambayo nitatoa ni yake,tuyachukulie kwa uzito wake,"amesema mhe.Dkt.Ndumbaro.
Amesema Makamu wa Rais ameqiza kongamano hilo lichukuliwe kwa uzito mkubwa kwani nyuma yake ni sehemu ya utekelezaji hasa kwa kuzngatia mkakati uliopo ni kutumia malighafi za ndani katika kuzalisha bidhaa na kwenye sekta ya misitu na nyuki kuna rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutumika viwandani.
"Kuna viwanda vingi ambavyo vinatumia malighafi za ndani, na hii sekta ya misutu na mazao yake inachangia katika pato la Taifa cha asilimia 3.5 ya pato la Taifa, na asilimia 5.9 ya mapato yatokanayo na biashara ya nje ya mazao ya misitu. Hivyo kongamano hili ni muhimu kwa mipango ambayo itasaidia kuiboresha sekta hii na kuongeza pato la taifa,"
Aidha ameagiza kuwepo na mkakati wa kuzitangaza bidhaa zinazotokana na uwepo wa misitu na nyuki, na amesisitiza kuna haja ya kuboresha ubora wa bidhaa huku akitaka kutatuliwa kwa changamoto zilizopo kwenye mnyororo wa thamani.
Akisoma hotuba hiyo ya Makamu wa Rais, Waziri Ndumbaro ameeleza kwamba nchini Tanzania kuna wasomi wengi ambao wanafanya tafiti katika misitu na nyuki lakini tafiti nyingi zinawekwa kwenye makabati,hivyo ameagiza zifike kwa wadau zikiwa katika lugha rahisi.
Pia amezungumzia changamoto mbalimbali ikiwemo ya uvamizi wa misitu ambao unasababishwa na kilimo, uchimbaji madini, ukataji mkaa, uchimbaji nguzo na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kupitia kongamano hilo ni vema wadau wakatafuta ufumbuzi wake.
Amewataka wadau hao kuchambua hotuba ya Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ambayo imezungunza kwa kina kuhusu sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya misitu hasa kutumia rasilimali za misitu katika kuongeza viwanda.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuongezwa kwa viwanda vingi nchini na watalaamu wanayo nafasi ya kujadiliana kwa kina na kisha kutoa ushauri kwa Serikali. "Katika misitu kuna viwanda zaidi ya 4000 lakini bado tija yake sio kubwa.
"Hata hivyo, uwekezaji huo umewezesha taifa kupunguza uingizaji wa bidhaa za mazao ya misitu toka meta za ujazo 95,000 mwaka 2015 hadi meta za ujazo 25,000 mwaka 2020. Huku biashara ya nje ikiongezeka toka meta za ujazo 33,000 hadi meta za ujazo 90,000 katika kipindi hicho, amesema Dkt.Ndumbaro wakati anasoma hotuba ya Makamu wa Rais.
Wakati huo huo amehimiza utunzaji wa mazingira kwani utunzaji wa mazingira ndio unaosababisha uwepo wa vyanzo vya maji, hewa safi ya oxijen ambayo ni ya bure inayotoka kwenye misitu."Iwapo tutatumia Oxygen inayotengenezwa na maabara basi kila Mtanzania kwa mwaka atatakiwa kutumia Sh. milioni 22.7.
"Ndio maana Makamu wa Rais anatuagiza tutunze mazingira maana hakuna uwezo wa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kununua hewa ya Oxygen. Tutunze mazingira yetu kwani faida zake ni nyingi,"amesema Waziri Ndumbaru.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema mipango hiyo aliyoizindua sasa ikawe chachu ya kuongeza ajira nchini na kuleta tija.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja amesema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali mbalimbali kwenye misitu na mazao yake pamoja na uwepo wa rasilimali kale na uoto wa asili.
Aidha, amewapongeza wadau wote ambao wamejikita katika kuendeleza na kusimmamia rasilimali za mazao ya misitu na nyuki, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza rasilimali za misitu na yakitunzwa vizuri matokeo yake ni makubwa
Kuhusu changamoto amesema shughuli za kibinadamu zimeendelea kuharibu rasimali za misitu huku akitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Watanzania kuhakikisha wanashiriki kutunza uoto wa asili kwani hivi sasa kumekuwepo na uharibifu mkubwa unatokana na uchomaji moto wa misitu.
"Naishukuru TAFORI kwa kuandaa kongamano hili, kwani kongamano hili ni moja ya njia ya kuwafikia wadau wote, na kwamba TAFORI wanalojukumu la kufanya tafiti katika eneo la Misitu, pamoja nyuki, hivyo kuna mipango miwili imeandaliwa kwa ajili ya sekta hizo mbili," amesema Mhe. Masanja.
Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFORI) Dkt.Revocatus Mushumbuzi amesema sekta ya misitu inauwezo mkubwa wa kuchangia uchumi wa nchi hii kutokana na uwepo wa misitu ya aina mbalimbali pamoja mashamba ya miti ya kupanda.
Amefafanua kuna faida nyingi za misitu ikiwemo kurekebisha mfumo wa hali ya hewa, utoaji ajira, uhifadhi wa ardhi na faida nyingine lukuki, hivyo Serikali iliona haja ya kuwa na TAFORI kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali pamoja na kusimamia misitu na mazao yatokanayo na misitu.
Kuhusu kongamano hilo amesema wameona kuna haja ya wadau kukutana kwa ajili ya kubadilisha mawazo kuhusu kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki.
Hivyo amesisitiza watatumia kongamano hilo kuangalia nini waendelee kufanya katika kuangalia mnyororo mzima wa misitu na nyuki pamoja ba kuonesha mchango wa hatua hizo katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu.
Hivyo mada kuu katika kongamano hilo ni mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki pamoja na kuangalia sera na sheria ambazo zinaendesha sekta hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam Kisari Makore ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakari Kunenge amesema amepata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika komangano hilo na ameshuhudia rasilimali za misitu na mazao ya nyuki, na kwake ni kama vile alikuwa anafanya utalii.
Hivyo amepongeza TAFORI kwa kuandaa kongamano hilo la Kimataifa kwani limekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia Serikali inaendelea na mikakati yake ya kuimarisha uchumi unaotokana na viwanda.
Amesema mazao ya misitu na nyuki ikipewa kipaumbele itakwenda kuimarisha uchumi unaotokana na rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo
Hata hivyo imefafanuliwa kwamba Mpango mkuu wa sekta ya nyuki unalenga kuotoa miongozo ya jumla katika sekta hiyo ili kuondoa au kupunguza changamoto zilizopo na hatimaye kuleta maendeleo kwa mtu moja kwa moja na taifa kwa ujumla. Ni mpango wa kwanza wa ufugaji nyuki ambao umegawanyika katika sehemu sita.
Kuhusu mpango wa utafiti wa misitu awamu ya tatu nao umejikita katika maeneo sita na kwamba mipango yote hiyo ni ya miaka 10 na baada ya hapo wataangalia kama imekidhi mahitaji au laa.