Resources » News and Events

Magogo ya Mkurungu kupigwa mnada Aprili 6, 2022

Magogo ya Mkurungu kupigwa mnada Aprili 6, 2022

Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) itapiga mnada magogo ya Mkurungu kwa njia ya kielectronic (mtandao) leo Aprili 6, 2022 kuanzia saa sita na dakika moja usiku (6:01) hadi saa saba kamili ya mchana (7:00).

Magogo hayo ya Mkurungu (Pterocarpus Tinctorius) vyenye jumla ya meta za ujazo 1,357.026 yapo katika eneo la Bandari Kavu lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Matumizi ya Rasilimali - TFS, Mhifadhi Mkuu, Salehe Beleko amesema leo Jumanne kuwa wametumia njia mbalimbali ili kufanikisha mnada huo kufanyika hasa kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Amesema ili kushiriki kwenye mnada, mshiriki alitakiwa kujisajili kupitia anuani ya http://mis.tfs.go.tz/e-auction ambapo mwisho wa kufanya usajili huo ilikuwa ni tarehe 3 Aprili, 2022 saa sita kamili usiku.

"Kazi yetu sisi TFS leo ni kupiga mnada kwa kuzingatia Kanuni ya 31 (ii) ya Kanuni za Sheria ya Misitu za Mwaka 2004," amesema Beleko.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Mhifadhi Mkuu Harold Chipanha anasema mfumo huo unaokwenda kutumika kuuza magogo hayo utamtambua mshindi na kumpa barua ya ushindi sambamba na hati ya madai ya asilimia 25 na 75 atakayotakiwa kulipa kupitia benki yake husika.

Anaongeza kuwa mshindi atapaswa kulipa asiliamia 25 ndani ya masaa 24 baada ya mnada kufungwa huku asilimia 75 zilizobaki akitakiwa kulipa ndani ya siku 14 za kazi.