WAZIRI mkuu mstaafu Mizengo Pinda ameupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kwa kazi kubwa inayofanya kuhamasisha ufugaji wa nyuki na na kuwawezesha wananchi ili waweze kujiongezea uchumi kupitia mazao yanayotokana na Nyuki.
Waziri Mkuu Mstaafu aliyasema hayo leo Mei 21, 2022 alipokuwa akikagua mabanda ya washiriki wa Maadhimisho ya siku ya Nyuki Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Azimio uliopo Mpanda Mkoani Katavi na kuhudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya chama na Serikali pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko .
Pinda ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha siku hiyo ya ufugaji Nyuki Duniani amesema awali TFS ilikuwa ikihamasisha wananchi kikamilifu namna ya ufugaji Nyuki hali iliyokuwa ngumu kueleweka kuliko iivyo sasa ambapo Wakala huo unazalisha bia mazao ya nyuki hai itakayowasaidia wananchi kujifunza kwa nadhalia na vitendo.
“TFS sasa SAFI! Naona mnazalisha mazao mbalimbali ya nyuki lakini kikubwa nimefurahi kuona mnazakisha chamvua, sasa muwahamasishe wafugaji kuvuna chamvua ili kujiongezea uchumi wa kifedha kwa kuwa zao hili lina thamani kubwa ukilinganisha na asali yenyewe,
“Mmeniambia hapa inawachukua siku saba uzalisha kilo moja na nusu ya chamvua kutoka kwenye mizinga 20 ambayo kilo hio mnauza kwa Tshs 300,000 hii ni habari njema, nilizoea kusikia Vumbi la Singida inayozalishwa na Kijiji cha Nyuki Singida sasa na nyie mmechangamkia fursa, sasa mvipe ujuzi huu vikundi mbalimbali vya ufugaji Nyuki,” anasema Pinda.
Amesema ili kufanikisha zoezi la ufugaji wa nyuki na kuvuna chamvua wafugaji wnatakiwa kuunda vikundi mbalimbali vya ufugaji Nyuki kisha vipatiwe elimu ya namna ya kufuga kwa mfumo wa kisasa na mwisho wa siku wanakuwa wafugaji bora wa wadudu hao ambao hutoa mazao mbalimbali ikiwemo zao la chamvua ambalo lina thamani kubwa na soko la uhakika ndani nan je ya nchi.
Aidha Pinda amepongeza kazi inayofanywa na Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kwa kulinda mapori mengi Tanzania na kuyafanya yaendelee kuwa na uoto wa asili jambo ambalo litaongeza uzalishaji wa mazao yanayotokana na Nyuki.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi anayesimamia rasilimali za nyuki Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Hussein Msuya amesema kuwa Wakala umejipanga vema kuhakikisha elimu inatolewa kwa wafugaji wa nyuki kwa nadhalia na vitendo.
Msuya anasema kwa kushirikia na Wizara kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya nyuki duniani, Mei 20, 2022 wamezindua kampeni ya kutundika mizinga katika msitu wa Manga mkoani Katavi ambapo jumla ya mizinga 40 ilitundikwa kwenye eneo hilo wakati TFS ikiendelea kuweka mpango utakaowezesha kuongezeka kwa mizinga hadi kufikia mizinga isiyopungua 270 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.