Resources » News and Events

Bodi ya Washauri TFS yaongezewa muda kutokana na usimamizi mzuri

BODI ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitatu, jambo ambalo limemfanya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro kuiongezea muda ili iendelee kutekeleza malengo ya Wakala sambamba na kuipatia maagizo kadhaa iyatekeleze.

Waziri Ndumbaro alisema Bodi imefanya kazi nzuri katika kuongeza mashamba ya misitu nchini, idadi ya viwanda vya mazao ya misitu vimeongezeka huku mchango wa mazao ya misitu katika uchumi wa nchi ukiongezeka sambamba na kuongeza ajira.

Akizungumza wakati wa kikao cha kuhitimisha muda wa Bodi hiyo na kuiongezea muda Desemba 19, 2021, Dk Ndumbaro alisema TFS ni miongoni mwa taasisi bora zinazotekeleza vyema majukumu yake chini ya wizara ambapo imekuwa miongoni mwa zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo.

Pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Brigedia Jenerali Mbaraka N. Mkeremy wajumbe wa Bodi hiyo waliiongezwa muda ni Piencia C. Kiure, Dk Siima S. Bakengesa, Dk Ezekiel E. Mwakalukwa, Injinia Enock E. Nyanda, Bahati L. Masila na Profesa Dos Santos A. Silayo ambaye ni kati wa Bodi.

Wajumbe hao wa Bodi waliteuliwa Desemba 19, 2018 kwa kipindi cha miaka mitatu hadi Desemba 18, Desemba, 2021 kwa mujibu wa Kifungu 6 (8) cha Sheria ya Wakala.

Akizungumza katika hafla hiyio, Dk Ndumbaro alisema anajivunia taasisi 17 kati ya 20 zilizopo chini ya Wizara, na küitaja TFS kuwa ya mfano kutokana na uwajibikaji katika masuala ya uhifadhi, upanuzi wa mashamba na uanzishaji mashamba mapya pamoja na kuanzisha huduma na bidhaa mpya ambazo zimekuwa zikiifanya kuwa ya mfano.

“Kwa kweli niwapongeze sana katika kazi mliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitatu. Nimefanya kazi katika bodi nyingi sana. Kwa hiyo majukumu ya bodi nayafahamu vizuri na niwapongeze kwa kutekeleza vizuri majukumu yenu vizuri,” alisema.

“Niwapongeze sana... niipongeze pia menejimenti chini ya uongozi wa Kamiashna wa Uhifadhi Profesa Dos Santos Silayo. Ndani ya wizara kuna tahsisi takriban 20, 17 zinafanya vizuri lakini TFS ni taasisi mojawapo inayofanya vizuri zaidi.”

Dk Ndumbaro alisema pamoja na mafanikio mengine, TFS ni kati ya taasisi ambazo zina migogoro michache zaidi kati ya 17 zinazofanya kazi, akisistiza kuwa kuna taasisi zingine zina wafanyakazi wachache kama 46 lakini zinakabiliwa na changamoto katika kuziongoza.

Alisema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unafanya kazi nzuri katika kanda zote na kwamba, anajivunia kuwa taasisi hii ni bora inayojiendesha vizuri katika wizara anayoiongoza.

Hata hivyo, Waziri Ndumbaro alionya kuwa hatasita kuchukua hatua iwapo kutajitokeza utendaji usiokuwa mzuri ndani ya TFS huku akiitaka menejimenti na Bodi kusimamia vizuri majukumu iliyokabidhiwa.

“Endeleeni kushikamana, endeleeni kusikiliza maelekezo ya Bodi,” alisema.

Akizungumzia kuiongezea muda Bodi, Dk Ndumbaro aliitaka iendelee kufanya kazi mpaka muda ambao Bodi mpya itateuliwa kuchukua nafasi ili kutokuwepo kwa ombwe la kiuongozi.

“Mtaendelea kutekeleza majukumu yenu mpaka hapo Bodi nyingine itakapotangazwa. Kama mna jambo la kutekeleza endeleeni kutekeleza. Kwa hiyo sitaruhusu kuwe na ombwe la uongozi…”