14
Feb

Tanzania yashiriki Warsha ya Urejesho wa Uoto wa Asili: Achieving AFR100 with Forest and Farm Producers Programme

Rome, Italia; Tanzania inashiriki katika warsha ya wiki moja ya urejeshaji wa Uoto wa Asiki inayofanyika makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome, Italia.

Warsha hio ilioanza Januari 09, 2025 inalenga kukamilisha mpango wa mradi unaojulikana kama Achieving AFR100 with Forest and Farm Producers Programme, mradi unaotekelezwa katika nchi sita, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Kenya, Togo, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Madagascar.

Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani (BMZ) kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 4.5 kwa kila nchi, huku FAO ikisimamia utekelezaji wa mradi huo. Lengo kuu ni kuhakikisha ufumbuzi endelevu katika urejesho wa uoto wa asili pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya watayarishaji wa mazao ya shambani na wale wanaohusika na misitu.

Katika muktadha wa Tanzania, utekelezaji wa mradi huu utafanyika katika maeneo mawili: uwanda wa Moduli-Babati na uwanda wa Zanzibar.

Tanzania inawakilishwa katika warsha hio na Mhifadhi Anna Lawuo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambaye pia amepewa jukumu la kuwa mratibu wa masuala ya urejesho wa uoto wa asili kwa nchi za Afrika Mashariki.

Mhifadhi Lauwo anasema, "warsha hii ni fursa muhimu ya kubadilishana mitazamo na mbinu bora kati ya washiriki wa nchi mbalimbali, na inatarajiwa kuimarisha jitihada za kulinda na kurejesha rasilimali asili, jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo endelevu".

Aliongeza kuwa, ushirikiano huu wa kimataifa unalenga kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa misitu na maeneo ya kilimo, huku ukileta pamoja wataalamu kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika ili kushirikiana katika utekelezaji wa malengo ya mradi.