24
Sep
NI SAO HILL MISITU SPORTS BONANZA 2026: MAPAMBANO YA UBINGWA KUANZA RASMI
Na Mwandishi Wetu – Iringa
Hamu ya mashindano imeanza kupanda katika Shamba la Miti Sao Hill, wilayani Mufindi, baada ya Wahifadhi wa Tarafa zote nne kupokea vifaa mbalimbali vya michezo, ikiwa ni ishara rasmi ya maandalizi ya kuanza kwa Sao Hill Misitu Sports Bonanza 2026 linalotarajiwa kuanza rasmi tarehe 1 Oktoba 2026.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa tarehe 25 Septemba,2026 kwa wawakilishi wa Tarafa za Mgololo, Irundi, Ihalimba na Ihefu, ambazo zitaingia uwanjani kuwania ushindi katika michezo mbalimbali itakayozikutanisha timu mbalimbali kutoka vijiji vinavyolizunguka Shamba la Miti Sao Hill.
Bonanza hilo linatarajiwa kuwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, marathon, mpira wa pete, kukimbiza kuku, draft, bao, darts,kuvuta kamba na mingine mingi huku hatua za awali za mtoano zikifanyika katika tarafa husika kabla ya timu na washiriki bora kusonga mbele kuelekea hatua za nusu fainali na fainali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu upande wa Uendelezaji wa Shamba PCO Saidi Singano awamewataka washiriki kujiandaa kikamilifu, kuzingatia nidhamu na kutumia bonanza hilo kwa kuendelea kueneza elimu ya kuzuia matumizi mabaya ya moto ambayo hupelekea uharibifu wa misitu.
Ameongeza kuwa huku elimu ya uhifadhi ikiendelea kutolewa, wananchi wataendelea pia kujenga afya, umoja, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi.
Kwa upande wao, wahifadhi wa Tarafa za Shamba la Miti Sao Hill wameeleza utayari wao wa kuingia uwanjani huku wakiahidi ushindani wa nguvu, wakisisitiza kuwa kila tarafa inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na lengo la kufikisha elimu ya uhifadhi na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Tarehe 1 Oktoba 2026, timu zitaanza kuchuana.
Michezo itaanza, ushindani utachukua nafasi na kila tarafa itapambana kutengeneza historia katika Sao Hill Misitu Sports Bonanza 2026.
" LINDA MISITU, ZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA MOTO"