Habari » News and Events

Waziri Makamba Aitaka NEMC Kuiga Utendaji wa TFS

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira ) Mhe. January Makamba (kushoto) akimkabidhi rasmi vitendea kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo mara baada ya kuzindua Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere leo tarehe 15, 2019.

Prof. Silayo ni miongoni mwa wajumbe nane walioteuliwa kuunda bodi ya NEMC itakayohudumu kwa kipindi cha miaka mitatu ikiwa chini ya mwenyekiti wake, Dkt. Flora Ismail Tibazwara.

Akiwakabidhi vitendea kazi (Sheria, Kanuni na Sera ya Mazingira) hivyo Mhe. Makamba aliitaka bodi hiyo kufanya mapinduzi ya kiutendaji kwa kuiga mfano wa TFS iliyoko katika wilaya zote nchini.

“Naamini mambo yatakwenda kubadirika sasa, NEMC kwa sasa inafanya kazi ya kutoa vyeti tu, sisemi hawafanyi kazi la hasha, wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni na taratibu lakini hawajajipambanua hivyo, sasa ibadirisheni NEMC iwe kama TFS, wao wapo kila wilaya hata kusiko na misitu, wapo kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni na taratibu; katika hili msiwe na shaka Serikali iko nyuma yenu” aliwasisitiza wajumbe wa bodi Mhe. Makamba.

Wajumbe wengine wanaounda Bbdi hiyo ni Prof. Hussen Sosovela, Dkt. Catherine Masao, Damas Masolongo, Dkt. Neduvoto Mollel, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa na Prof. William Mwigoha.