WANANCHI WATAKIWA KUPANDA MITI KWA AJILI YA KIZAZI CHA SASA NA KIJACHO

JUU PICHANI: Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill Tarafa ya Kwanza Irundi Bi. Glory Fortunatus akitoa maelezo wa viongozi mbalimbali kutoka mkoani Geita waliofika kwenye ziara ya mafunzo katika bustani ya  miche iliyopo katika tarafa hiyo jana.

Viongozi wa Wilaya, Mkoa wa Geita, na vijiji vinavyozunguka Shamba la Miti la Biharamulo mkoani Geita wamewataka wananchi kupanda miti kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae. Hayo yamesemwa na viongozi hao mara baada ya kutembelea Shamba la Miti Sao Hill linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji katika shamba hilo. Kiongozi wa msafara huu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Eng. Mtemi Msafiri anasema wameona ni vyema kujifunza katika shamba hilo kwa sabababu ndilo shamba kongwe na kubwa zaidi miongoni mwa mshamba yanayosimamiwa TFS. “Shamba la Miti Sao Hill ndilo shamba kubwa zaidi kati ya mashamba yote ya Serikali na ni nguzo ya maendeleo, na mkombozi wa mazingira wa Wilaya ya Mufindi na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nasi tumeona ni vema tujifunze kutoka kwa wenzetu.

“Tumejionea jinsi shamba hili lilivyo kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa mbao, linavyosaidia kuongezeka kwa ari ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wanaozunguka shamba, lakini pia tumeelezwa kuwa wananchi wa Wilaya za Mufindi, Kilombero na jamii jirani wamekuwa wakipatiwa gawio la asilimia 5 ya mrahaba kila mwaka. Ni wazi shamba hili lina mchango mkubwa katika maendeleo nasi tunataka haya yatokee kwa wananchi wetu ndio mana tuko hapa kujifunza, “anasema Mhe Eng. Msafiri. Mhe Eng. Msafiri anasema ziara hiyo imeweza kuwafumbua macho na kuona jinsi gani shamba hilo lilivyo toa fursa ya ajira zinazotokana na kazi za msimu za mashambani na viwanda tegemezi vya mazao ya misitu, fursa za uwekezaji, na ufugaji wa nyuki unaotokana na na uwepo wa misitu ya asili na ile ya kupandwa pamoja na vyanzo mbalimbali vya maji.

PICHANI: Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu na Nyuki TFS,  Zawadi Mbwambo akiwaeleza tofauti ya mche wa mkaratusi ulioboreshwa alioushika na ile ambayo haijaboreshwa kwa viongozi waliofika ziarani jana

Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu na Nyuki TFS, Zawadi Mbwambo amesema shamba hilo limehamasisha kwa kiwango kikubwa upandaji wa miti kwa jamii inayolizunguka ambapo pia hutoa msaada wa mafunzo na miche ya miti kwa ajili ya kupandwa ili kupambana na uharibifu mkubwa wa misitu unaoendelea nchini. “Takribani hekta 372,000 ya misitu inapotea kila mwaka na ili misitu hii isiweze kupotea tunatakiwa tuendelee kupanda angalau hekta 185,000 kwa mwaka kwa hapa Mufundi na Ukanda wote wa Nyanda za Juuu Kusini hamasa ya kupanda miti imekuwa kubwa kutokana na thamani inayoonekana Sao Hill kiasi kwamba imefikia hatua sasa Serikali inawaelimisha watu waache baadhi ya maeneo kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara” Alisema Mbwambo.

Kwa upande wake meneja wa Shamba la Miti la Biharamulo Thadeus Shirima anasema kupitia ziara hiyo ya siku mbili anaamini sasa kutakuwa na uelewa wa pamoja wa umuhimu wa shamba hilo katika kuleta maendeleo katika Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla. Thadeus alitoa shukurani kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Chato na Mkoa wa Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Bukombe kwa msaada na maelekezo yao muhimu yaliyosaidia kuhakikisha uanzishwaji wa Shamba la Miti la Biharamulo unafanikiwa kwa kufanikisha kuwaondoa wananchi waliovamia msitu wa hifadhi Biharamulo ili kuanzishwa shamba hilo la miti. Ziara hiyo ina wajumbe 45 ambao vingozi wa Wilaya na Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mkurugenzi wa halmashauri , Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Maafisa tarafa, Jeshi la Zima moto na uokoaji, Mwenyekiti na katibu wa Chama cha Mapinduzi, baadhi ya Wakuu wa Vitengo na Idara za Halmashauri ya Wilaya, baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya , Katibu Tawala wa Wilaya na Wataalamu kutoka Shamba la miti Biharamulo.