Makamu Wa Rais Atembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo ameendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro ambapo mapema hivi leo alitembelea ofisi ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kupokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Sanatos Silayo na kuzindua ofisi za hifadhi hiyo.

Akimkaribisha Makamu wa Rais kuzindua jingo hilo, Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo alisema katika kipindi cha miaka 3 tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano kumekuwa na mafanikio na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali.

“TFS mengi hasa katika ujenzi wa majengo ambapo leo unatuzindulia moja kati ya majengo mapya 40 (ofisi 12, nyumba za watumishi 13, ranger out posts 15) tuliyojenga katika maeneo mbalimbali nchini,”

“Ofisi ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome unayoizindua hivi leo ni moja kati ya ofisi hizo zilizojengwa katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,” alisema Mbwambo.

Mbwambo anasema sambamba na ujenzi wa majengo hayo TFS imekarabati majengo 224, barabara mpya za kilomita 240 zimefunguliwa katika misitu mbalimbali nchini huku kilomita 3,184 zikikarabatiwa.

Katika uzinduzi huo viongozi mbalimbali wa nchi wakiongozwa na Makamu wa Rais walipanda fursa ya kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.