Kwa nini Serikali imeamua kuilinda Misitu kijeshi?

Misitu inatajwa kuwa ndiyo rasilimali muhimu kuliko zote duniani katika maisha ya binadamu, lakini ndiyo inayoongoza kuathiriwa na kuharibiwa kwa kasi kubwa na watu.

Umuhimu wa misitu unatokana na kuwa chanzo cha uhai wa viumbe na hivyo ni vyema ikahifadhiwa ili maisha yaendelee kuwapo duniani.

Kama ilivyo katika nchi nyingi duniani, misitu imekuwa ikiharibiwa kwa kiwango cha kutisha, jambo linaloibua hofu ya kuwapo tishio la janga la kibinadamu katika miaka ya usoni litakalotishia uhai wa binadamu na viumbe.

Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 94,500 (hekta milioni 94.5), kati ya hizo eneo la misitu ni takribani hekta milioni 48.1. Kulingana na kigezo cha uhifadhi, takribani hekta milioni 28 ni hifadhi maalumu kwa ajili ya maji, baioanuwai na ardhi huku eneo la misitu lililosalia likiwa ni hifadhi na matumizi endelevu.

Kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya rasilimali za misitu iliyofanyika mwaka 2009-2014 iliyotolewa na Wizara ya Malisili na Utalii kupitia Taarifa ya Tathmini ya Rasilimali za Misitu (Naforma), moja ya tatu ya eneo lililofunikwa na misitu linamilikiwa na Serikali kuu katika takribani misitu 500, huku mbili ya tatu likiwa chini ya usimamizi wa Serikali za mitaa yaani misitu 231, vijiji na sekta binafsi.

Licha ya utajiri huo wa misitu, uharibifu wa misitu ni mkubwa hapa nchini kama anavyosema mtendaji mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo.

Anasema misitu inakabiliwa na changamoto nyingi ambapo kuanzia Kanda ya Ziwa kuelekea Kusini inaathiriwa na tabiachi, shughuli za kibinadamu kama ukataji wa miti kwa ajili ya nishati, mbao, kilimo cha kuhamahama na kadhalika.

“Zipo pia shughuli za ufugaji, uchimbaji madini na uvamizi wa misitu, moto unaoanzishwa na watu mbalimbali. Tunapaswa tuweke mikakati ya kuutokomeza,” anasema Profesa Silayo.

Ulinzi wa misitu;

Kwa mujibu wa Profesa Silayo, TFS kama taasisi ya Serikali iliyokabidhiwa jukumu la kuhakikisha uhifadhi endelevu wa misitu nchini, watailinda misitu na mazao yake kwa kila hali bila kuchoka.

Profesa Silayo anasema mabadiliko yanayotarajiwa kuifanya TFS kuwa mamlaka kamili yatawapa nguvu kubwa kukabiliana na waharibifu wa misitu na mazao yake, na pia uhifadhi wenye tija kubwa kwa Taifa.

“Tumejipanga kwa hilo, jeshi (usu) hili litakuwa mhimili wa kuhahakisha kwamba misitu yetu iko salama, tunawaomba wananchi watuunge mkono,” alisema Profesa Silayo katika ufungaji wa mafunzo ya maofisa 140 wa jeshi usu yaliyofanyika Mlele mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu anasema Serikali iko katika hatua za mwisho za kuruhusu matumizi ya silaha za moto kwa maofisa wa jeshi hilo litakalolinda misitu na mazao yake, na kuhakikisha uwapo wa uhifadhi endelevu wa maeneo hayo.

“Leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli wa TFS, lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinasababisha uharibifu mkubwa sana wa mazingira na hatuwezi kusema zisiendelee, zinatakiwa kuendelea katika namna ambayo haitaifanya nchi yetu kuwa jangwa,” alisema Kanyasu wakati akiwaapisha askari hao.

Kanyasu alisema, “kuhitimu kwenu hakumaanishi mnakwenda kuzuia maendeleo, kunamaanisha mnakwenda kushirikiana na wanaotaka maendeleo kwa kufanya kazi wakifikiria maendeleo endelevu.”

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Antonia Kapanya alisema wamejifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na majangili wa misitu na mazao yake na kwamba, wanachoomba ni Serikali kuwaruhusu na kuwapatia silaha ili waweze kutekeleza ipasavyo majukumu yao.

“Tunaomba kupatiwa silaha za moto ili kukabiliana na majangili, maana wapo wanaokuwa nazo,” alisema, suala ambalo  Kanyasu alisema Serikali inalishughulikia.

Kaimu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kemilembe Luota alisema wataendelea kuishauri Serikali namna bora ya kukabiliana na uharibifu wa misitu na uhifadhi.